"Nakubali makosa yangu" Mason Greenwood azungumza baada ya mkataba wake na Man U kukatizwa

Alisisitiza kuwa hana hatia na kubainisha kuwa hakufanya makosa mbalimbali ambayo alishutumiwa mwaka jana.

Muhtasari

•Greenwood alisema kuwa uamuzi wa kuondoka Man United ulifuatia mashauriano kati yake, familia yake na klabu.

•Greenwood alikiri katika  siku za nyuma aliwahi kufanya makosa katika mahusiano yake, ambayo anasema sasa amejifunza nayo na yuko tayari kubadilika.

Mshambulizi wa United Mason Greenwood ashtumiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kinyumbani
Mshambulizi wa United Mason Greenwood ashtumiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kinyumbani
Image: HISANI

Mshambulizi wa Uingereza Mason Greenwood amethibitisha kuondoka katika klabu ya Manchester United baada ya mashtaka ya makosa ya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji dhidi yake kuondolewa mapema mwaka huu.

Katika taarifa ya Jumatatu, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alisema kuwa uamuzi wa kuondoka Man United ulifuatia mashauriano kati yake, familia yake na klabu hiyo yenye maskani yake jijini Manchester.

Greenwood alitoa shukrani zake kwa Mashetani Wekundu kwa kumpa jukwaa la kuonyesha ujuzi wake wa soka  kwa takriban miaka 14 iliyopita na kusisitiza kuwa klabu hiyo itasalia milele moyoni mwake.

"Uamuzi wa leo umekuwa sehemu ya mchakato wa ushirikiano kati ya Manchester United, familia yangu na mimi. Uamuzi bora kwetu sote, ni mimi kuendelea na maisha yangu ya soka nje ya Old Trafford, ambapo uwepo wangu hautakuwa kikwazo kwa klabu. Ninashukuru klabu kwa usaidizi wao tangu nilipojiunga na umri wa miaka saba. Siku zote kutakuwa na sehemu yangu ambayo ni United,” Greenwood alisema.

Pia alifichua mipango yake inayofuata ambapo alidokeza kuwa ana mpango wa kuendelea kucheza soka na pia kubadilika na kuwa mtu bora.

"Ninashukuru sana familia yangu na wapendwa wangu wote kwa msaada wao, na sasa ni kwangu kulipa imani ambayo wale walio karibu nami wameonyesha. Nina nia ya kuwa mwanasoka bora, lakini muhimu zaidi baba mzuri, mtu bora, na kutumia vipaji vyangu kwa njia chanya ndani na nje ya uwanja,” alisema.

Mshambulizi huyo alisisitiza kuwa hana hatia na kubainisha kuwa hakufanya makosa mbalimbali ambayo alishutumiwa mwaka jana.

Hata hivyo alikiri kwamba katika  siku za nyuma aliwahi kufanya makosa katika mahusiano yake, ambayo anasema sasa amejifunza nayo na yuko tayari kubadilika.

“Naelewa kuwa watu watanihukumu kutokana na walichokiona na kusikia kwenye mitandao ya kijamii, na najua watu watanifikiria vibaya zaidi. Nililelewa kujua kwamba unyanyasaj katika uhusiano wowote ni mbaya, sikufanya mambo niliyoshtakiwa, na Februari niliondolewa mashtaka yote.

Walakini, ninakubali kabisa nilifanya makosa katika uhusiano wangu, na ninachukua sehemu yangu ya uwajibikaji kwa hali zilizosababisha chapisho la media ya kijamii. Ninajifunza kuelewa majukumu yangu ya kuweka mfano mzuri kama mchezaji wa kulipwa, na ninaangazia jukumu kubwa la kuwa baba, na pia mshirika mzuri, " Greenwood alisema.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 21 alifutiwa mashtaka ya unyanyasaji na ubakaji mwezi Februari mwaka huu baada ya kushtakiwa na mpenzi wake mapema mwaka jana.