Wapenzi wa soka waisuta Man United kwa kumsitisha mkataba wa Greenwood

“Kwa ishara zote huu uamuzi huenda umechochewa na ubaguzi wa rangi, mnamfukuza kwa sababu ni nusu Mwafrika,” mwingine alisema.

Muhtasari

• Hata hivyo, mashabiki wa soka mitandaoni walihisi kwamba uamuzi wa United kumfukuza kinda wao ulikuwa wa kuchochewa.

• Mwezi Februari mwaka huu hata hivyo Mahakama ilimuondolea tuhuma zote Greenwood baada ya kubaini kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumweka hatiani.

Mason Greenwood
Image: kwa hisani

Aliyekuwa kinda wa Manchester United Mason Greenwood ametoa kauli yake saa chache baada ya klabu hiyo kutangaza uamuzi mgumu wa kusitisha kandarasi yake.

Mason Greenwood alijipata kwenye mkondo wa matatizo mwaka jana kufuatia picha na video za mpenzi wake aliyezivujisha akimtuhumu kinda huyo kwa kumdhulumu kijinsia katika mzozo wa kinyumbani.

Mwezi Februari mwaka huu hata hivyo Mahakama ilimuondolea tuhuma zote Greenwood baada ya kubaini kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumweka hatiani.

Hata hivyo, hakuweza kurejeshwa katika kikosi cha The Red Devils kufuatia pingamizi kali kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa kike wa timu hiyo, jambo lililopelekea uongozi wa United kuanzisha uchunguzi wao wa ndani ili kubaini hatua madhubuti za kuchukua.

Baada ya uchunguzi huo uliochukua miezi kadhaa, Jumatatu alasiri United walitoa taarifa kwamba wameafikiana kusitisha kandarasi ya Greenwood na kumruhusu kuondoka kwenye timu yao ili kujiendeleza kwingineko mbali na Old Trafford.

“Mason leo amekiri bayana kwamba alifanya makosa ambayo atayajukumikia mwenyewe. Wale wote waliohusika akiwemo Mason wametambua kwamba kuna ugumu kwake yeye kuweza kuendelea taaluma yake katika klabu ya Manchester United. Kwa hiyo imeafikiwa kwa maamuzi ya pande zote kwamba ni vyema kwake kuiendeleza taaluma yake mbali na Old Trafford,” sehemu ya taarifa ya klabu ilisoma.

Greenwood kwa upande wake alikiri kwamba ni kweli umekuwa wakati mgumu sana na kusema kwamba ameona ni vyema aache kuisumbua United kwani kumekuwa na mihemko nje ya uwanja huo wakishinikiza kufukuzwa kwake.

“Nataka kuanza nikisema kwamba najua watu watanihukumu kwa kile ambacho wameona katika mitandao ya kijamii na najua wengi watanifikiria kwa ubaya. Ninajifunza kukubali majukumu yangu na kuwa mfano mwema katika taaluma ya soka, na pia nimezingatia katika jukumu kubwa la kuwa baba bora na pia mwenzi mwema,” Greenwood alianza katika barua yake.

“Uamuzi wa leo umekuwa moja kati ya suluhu nyingi kati ya Manchester United, familia yangu na mimi. Uamuzi bora kwetu sote ni mimi kuendeleza soka langu mbali na Old Trafford, sehemu ambayo kuonekana kwangu hakutadhuru klabu,” Greenwood aliendelea akitoa shukrani zake kwa United ambayo alijiunga akiwa na umri wa miaka 7.

Hata hivyo, mashabiki wa soka mitandaoni walihisi kwamba uamuzi wa United kumfukuza kinda wao ulikuwa wa kuchochewa na ubaguzi wa rangi ikizingatiwa kwamab kijana huyo ana chembechembe za Kiafrika.

Wengine walihisi kwamba kijana huyo alistahili kupewa nafasi ya pili timuni, haswa baada ya mahakama kumuondolewa mashtaka.

Haya hapa ni maoni ya baadhi ya mashabiki.

“Mimi pia ninaondoka katika klabu hii ikizingatiwa kwamba hawapatii mtu nafasi ya pili kujirudi. Watu hufanya makosa, huyu alistahili msamaha,” Holli Trigga alisema.

“Nimekuwa shabiki wa United kwa miaka 18 na inaonekana kwamba huu ndio uamuzi mbaya Zaidi. Mimi nilimuaminia kijana huyu, mimi nadhani Man U kinadharia wanatufukuza sisi mashabiki, hawaonekani kuwa na maslahi yetu moyoni, ni vibaya,” Eric Eru alizomea.

“Kwa ishara zote huu uamuzi huenda umechochewa na ubaguzi wa rangi, mnamfukuza kwa sababu ni nusu Mwafrika,” mwingine alisema.