Kwa nini EPL wamegoma kukubali Chelsea kuchapisha nembo ya mdhamini mpya kwenye jezi?

Kampuni ya Infinite Athlete inayotaka kufadhili Chelsea inatajwa kuwa na mauzo ya £12m licha ya kuwa na makubaliano ya kufadhili Chelsea kwa £40m kwa msimu, jambo ambalo limeleta mkwamo.

Muhtasari

• Hivyo, EPL wanaitaka Infinite Athlete kutoa hakikisho kwa njia ya nyaraka za maandishi kudhibitisha ufadhili wao.

• Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Chelsea Chris Jurasek, ambaye alikuwa afisa mkuu wa klabu ya Clearlake, anafahamika kufanyia kazi mpango huo.

Chelsea bila mfadhili
Chelsea bila mfadhili
Image: Chelsea

Kwa takribani mwezi mmoja sasa klabu ya Chelsea imekuwa ikisemekana kwamba imeshapata mfadhili mpya lakini bado hawajakubaliwa na uongozi wa ligi ya Premia kuchapisha nembo ya mfadhili huyo kwenye sehemu ya mbele ya jezi zao za msimu huu.

Kwa mujibu wa Evening Standard, Chelsea wanasubiri Ligi Kuu kuidhinisha mkataba wao wa udhamini wa pauni milioni 40 kwa mwaka na kampuni ya data za michezo ya Infinite Athlete.

Jarida hilo linadai kwamba mkwamo huo baina ya EPL na Chelsea umetokana na kugunduliwa kwamba kampuni hiyo ya Infinite Athlete ilianzishwa wiki moja tu kabla ya majadiliano kuhusu kuifadhili Chelsea.

Infinite Athlete wanatajwa kuwa na faida ya mauzo yenye thamani ya pauni milioni 12 tu licha ya kukubaliana na Chelsea kuhusu mkataba wa kuwafadhili kwa pauni milioni 40 kwa kila msimu.

Hivyo, EPL wanaitaka Infinite Athlete kutoa hakikisho kwa njia ya nyaraka za maandishi kudhibitisha ufadhili wao na wapi watapata kiasi hicho kingine cha fedha kufanikisha mkataba wenyewe.

Uanzishaji huo unalenga kudhibitisha kuwa umeongeza ufadhili mkubwa kupitia mtaji wa ubia na una nia ya kutumia udhamini wa Chelsea kuzindua chapa yake ulimwenguni.

Pia kuna wasiwasi kama mkataba huo utapitisha sheria za "soko la haki" za Premier League, huku mfadhili wa Infinite Silver Lake akihusishwa na Clearlake Capital, mmiliki wa hisa nyingi katika Chelsea.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Chelsea Chris Jurasek, ambaye alikuwa afisa mkuu wa klabu ya Clearlake, anafahamika kufanyia kazi mpango huo.

Jurasek analenga kumaliza msururu wa mechi zisizo na wafadhili kwa Chelsea, ambao huenda wakakabiliana na Luton kwenye Ligi ya Premia wakiwa na jezi tupu Ijumaa usiku.

Hii inafuatia Chelsea kujiondoa katika mkataba na kampuni ya kamari ya Stake.com kufuatia hisia hasi za mashabiki na Ligi ya Premia kuzuia makubaliano na Paramount+ kwa wasiwasi kwamba mpango huo ungekiuka sheria zinazowalinda wamiliki wa haki za TV kwenye ligi hiyo.