Tuzo za PFA: Timu Bora ya Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2022/23 yatajwa, wafahamu washindi wote

Wachezaji bora wa msimu uliopita walitunukiwa tuzo katika vipengele tofauti wakati wa hafla hiyo iliyowakutanisha mastaa wa klabu mbalimbali.

Muhtasari

•Mshambulizi Erling Haaland anayechezea klabu ya Manchester City alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA.

•Washambulizi Harry Kane wa Tottenham, Erling Halaand wa Man City na Bukayo Saka wa Arsenal walishirikishwa kwenye timu hiyo.

Lauren James, Erling Haaland na Bukayo Saka wakiwa na tuzo zao.
Image: TWITTER// PFA

Hafla ya tuzo za PFA (Professional Footballers’ Association) ilifanyika katika ukumbi wa Lowry Theatre mjini Manchester, Uingereza Jumanne siku ya jioni, Agosti 29.

Wachezaji bora wa msimu uliopita wa ligi mbalimbali nchini Uingereza walitunukiwa tuzo katika vipengele tofauti wakati wa hafla hiyo iliyowakutanisha mastaa wa klabu mbalimbali.

Mshambulizi matata kutoka Norway, Erling Haaland anayechezea klabu ya Manchester City alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA baada ya kuibuka mfungaji bora katika EPL 2022/23 na Ligi ya Mabingwa. Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 23 alifunga mabao 36 katika Ligi Kuu ya Uingereza, mabao 12 katika Ligi ya Mabingwa, 3 katika FA na bao moja kwenye Kombe la Carabao.

Bukayo Saka wa Arsenal alishinda tuzo la Mchezaji Chipukizi Bora wa Mwaka wa PFA baada ya kufunga mabao 14 na kutoa asisti 11 katika msimu uliopita. Winga huyo mwenye umri wa miaka 21 pia aliwasaidia wanabunduki kumaliza katika nafasi ya pili katika msimu wa Ligi Kuu ya 2022/23.

Rachel Daly anayechezea Timu ya Wanawake ya Aston Villa alishinda tuzo la Mchezaji Bora wa PFA kwa ligi ya wanawake huku Lauren James wa Chelsea akiondoka na tuzo la Mchezaji Chipukizi wa PFA kwa ligi hiyo hiyo.

Washindi wengine ni Chuba Akpom wa Ajax aliyeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Wachezaji wa Championship wa PFA, Conor Chaplin wa Ipswich Town aliyezawadiwa Mchezaji Bora wa mwaka wa PFA League One na Andy Cook aliyeshinda Ligi ya PFA ya Mchezaji Bora wa Leaugue Two.

Kikosi bora cha mwaka cha PFA Premier League kilijumuisha mlinda mlango wa Arsenal Aaron Ramsdale, mabeki John Stones, Ruben Dias, William Saliba na Kieran Trippier. Viungo wa kati walikuwa Rodri wa Manchester City na Martin Odegaard wa Arsenal huku Harry Kane wa Tottenham Hotspurs, Erling Halaand wa Man City na Bukayo Saka wa Arsenal pia wakishirikishwa kwenye timu hiyo.

Mwimbaji wa Nigeria Davido alichaguliwa kuwatumbuiza wageni katika hafla hiyo.