Wanaharakati Uhispania wataka Getafe kumfukuza Greenwood siku 2 baada ya kumsaini

"Watendaji wa Getafe hawakupaswa kamwe kumwajiri Mason Greenwood na wanapaswa kubatilisha uamuzi wao mara moja..."

Muhtasari

• Hakuna kisingizio cha kuchukua msimamo usioegemea upande wowote kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake - ilisoma taarifa.

Mason Greenwood kubadili uraia
Mason Greenwood kubadili uraia
Image: BBC NEWS

Mashirika ya  kuendesha kampeni dhidi ya unyanyasaji wa kinyumbani nchini Uhispania yameripotiwa kujitokeza bayana na kutoa taarifa kwa klabu ya soka ya Getafe kumfukuza mshambuliaji Mason Greenwood siku mbili tu baada ya kumsaini.

Mchezaji huyo amekuwa akiandamwa na masaibu si haba tangu mwaka jana mrembo wake alipotoa video na picha akionesha jinsi Greenwood alivyomdhulumu katika mzozo wa kinyumbani.

Hata baada ya kupatikana bila hatia na mahakama nchini Uingereza mwezi Februari mwaka huu, klabu ya Manchester United ilidinda kumrejesha kwenye kikosi cha kwanza kufuatia maandamano na pingamizi kali kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa kike.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, United hatimaye ilitangaza kuwa haingeweza tena kumrejesha Greenwood katika timu hiyo ikisema kuwa pande zote zimeafikiana kuukatisha mkataba wake hivyo Greenwood akawa mchezaji huru.

Timu nyingi barani ulaya zilionesha kudinda kumchukua kinda huyo mwenye kipaji lakini Katika siku ya mwisho ya uhamisho, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alifanikiwa kukamilisha uhamisho wa mkopo kwa timu ya La Liga, Getafe.

Hata hivyo, baada ya kupata saini ya Greenwood, upande wa Uhispania umekuwa ukichunguzwa vikali, kulingana na Daily Mirror.

Chapisho hilo linaripoti kwamba Wakfu wa Ana Bella, shirika la usaidizi la unyanyasaji wa nyumbani nchini humo, limeomba rasmi klabu hiyo kufikiria upya uamuzi wa kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa United.

Taasisi hiyo inaripotiwa kuwakosoa Getafe kwa 'kuweka mfano mbaya' kwa kuleta Greenwood, kama Manchester Evening News pia ilivyoripoti.

"Watendaji wa Getafe hawakupaswa kamwe kumwajiri Mason Greenwood na wanapaswa kubatilisha uamuzi wao mara moja. Ikiwa wewe ni shirika linalotazamana na umma kama Getafe, hakuna kisingizio cha kuchukua msimamo usioegemea upande wowote kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake - lazima uchukue jukumu la kimaadili."

Greenwood amekuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi 18 kutokana na madai ya kujaribu kumshambulia na kudhibiti tabia zinazoelekezwa kwake.