Kwa mara nyingine tena staa wa Ureno wa muda wote Christiano Ronaldo amezungumzia kile kinachochukuliwa na mashabiki wengi wa kandanda kama uhasama wa kisoka baina yake na Lionel Messi kutoka Argentina.
Ronaldo aliulizwa iwapo yeye na Messi ni maadui katika malimwengu ya soka jambo ambalo alilikanusha vikali akisema kuwa hakuna haja kwa mashabiki wake kumchukia mwenzake Messi.
Alisema kwamba yeye na Messi japo si marafiki lakini wanaheshimiana pakubwa, akisema kwamba pamoja walishiriki katika jukwaa moja la kupambania tuzo mbali mbali duniani kwa Zaidi ya miaka 15 na hivyo hakuna haja ya watu kuhisi kama kuna uadui baina yao.
“Ushindani? Sioni mambo kama hayo, tulishiriki jukwaa kwa miaka 15, sisemi ni marafiki, lakini tunaheshimiana. Ushindani ulikuwa mzuri, mashabiki walipenda." Alisema.
Nahodha huyo wa Ureno na Al Nassr alisema kwamba kama kweli mashabiki wake wanamkubali basi hakuna haja yoyote ya kumchukia Messi kwani nia yao katika soka ni kuleta mihemko ya furaha kwa mashabiki uwanjani na wala si kujaribu kuzushiana uadui.
“Ikiwa unampenda Cristiano, si lazima umchukie Messi. Wawili hao walibadilisha historia ya soka na wanaheshimika. Ushindani umekwisha. Sote wawili tumekuwa tukifanya mambo vizuri (nchini Uarabuni na MLS),” aliongeza.
Kauli hii ya Ronaldo inakuja saa chache baada ya UEFA kutoa orodha kamilifu ya wachezaji 30 ambao watashiriki katika kuwania tuzo ya Ballon d’Or.
Kwa mara ya kwanza katika miaka 20, Ronaldo alifungiwa nje ya orodha hiyo huku Messi akiteuliwa.
Endapo atashinda tuzo hiyo, Messi ataweka rekodi kwa kuishinda mara 8, rekodi ambayo haijawahi wekwa na mchezaji yeyote.
Ronaldo ameshinda Ballon d’Or mara 6.