Man United yavunja kimya kuhusu hatima ya Anthony, yamzuia kurejea mazoezini

Klabu hiyo ililaani vikali vitendo ambavyo Antony anatuhumiwa kumtendea aliyekuwa mpenzi wake.

Muhtasari

•Man U ilitangaza kwamba Anthony hatarejea kwenye mazoezi Jumatatu pamoja na wachezaji wengine ambao hawakushiriki mechi za kimataifa.

•Anthony anatarajiwa kujieleza kuhusu tuhuma za shambulio zinazomkabili kabla ya kuruhusiwa kurejea klabuni.

Image: INSTAGRAM// ANTHONY

Klabu ya Soka ya Manchester United hatimaye imevunja ukimya kuhusu suala linalomhusu mmoja wa wachezaji wake, Mbrazil Anthony Matheus dos Santos.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili jioni, klabu hiyo ilitangaza kwamba Anthony hatarejea kwenye mazoezi Jumatatu pamoja na wachezaji wengine ambao hawakushiriki mechi za kimataifa lakini badala yake atachelewesha kurejea kwa kipindi kisichodhihirishwa.

Man U ilidokeza kuwa winga huyo mwenye umri wa miaka 23 anatarajiwa kujieleza kuhusu tuhuma za shambulio zinazomkabili kabla ya kuruhusiwa kurejea klabuni.

“Manchester United inatambua madai yaliyotolewa dhidi ya Antony. Wachezaji ambao hawajashiriki katika mechi za kimataifa wanatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu. Hata hivyo, imekubaliwa na Antony kwamba atachelewesha kurejea kwake hadi taarifa nyingine ili kushughulikia madai hayo,” ilisema taarifa ya Manchester United.

Klabu hiyo iliendelea kulaani vitendo ambavyo Antony anatuhumiwa.

"Kama klabu tunalaani vitendo vya dhuluma na unyanyasaji. Tunatambua umuhimu wa kuwalinda wale wote wanaohusika katika hali hii, na tunakubali athari zinazotokana na tuhuma hizi kwa waathirika wa unyanyasaji,” ilisema taarifa hiyo.

Wiki iliyopita, Antony aliondolewa kwenye kikosi cha Brazil kufuatia madai ya unyanyasaji wa nyumbani ambayo mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 23 alishtumiwa na mpenzi wake wa zamani Gabriela Cavallin.

Katika taarifa, timu ya taifa ya Brazil ilisema kuwa nia ya kumuondoa mchezaji huyo wa zamani wa Ajax kwenye kikosi ni kumlinda mwathiriwa.

“Kutokana na ukweli uliojidhihirisha hadharani Jumatatu hii (Septemba 4), ukimhusisha mshambuliaji Antony, kutoka Manchester United, na ambao unatakiwa kuchunguzwa, na ili kumhifadhi mwathiriwa, mchezaji, timu ya Brazil na CBF, shirika linaarifu kwamba mwanariadha huyo ameondolewa katika timu ya Brazil,” taarifa ya timu ya taifa ya Brazil ilisoma.

Kujaza nafasi yake, Kocha Fernando Diniz alimuita Gabriel Jesus wa Arsenal, ambaye alichaguliwa kabla ya orodha ya wachezaji 36 iliyotumwa kwa  FIFA.

Katika shutuma zake, Bi Gabriela Cavallin anadai kwamba Antony alimshambulia mara kadhaa kati ya Juni 2022 na Mei mwaka huu.

Katika mahojiano na UOL, DJ huyo alidai kuwa Antony alishambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Brazil mnamo Juni 1 2022 akiwa mjamzito walipokuwa likizoni . Anadai alitishia kumtupa kutoka kwa gari linaloenda.