Manchester United italazimika kucheza bila huduma za nyota wao Antony itakapochuana na Brighton siku ya Jumamosi.
Mbrazil huyo ambaye anashughulikia tuhuma za unyanyasaji wa nyumbani amepewa likizo ili kushughulikia changamoto anazo kabiliana nazo.
Vijana hawa wa Erik ten Hag wamepoteza michezo miwili kati ya minne ya ufunguzi wa Premier League, huku mazozano yakiendelea dhidi ya wamiliki wa familia ya Glazer, ambao wanaonekana kusimamisha jaribio lao la kuiuza klabu hiyo.
Antony aliondolewa kwenye kikosi cha Brazil mapema mwezi huu kufuatia madai ya kushambuliwa kwake na mpenzi wake wa zamani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, aliyesajiliwa kutoka Ajax kwa pauni milioni 86 ambazo ni sawa na (dola milioni 107) mwaka jana, amekanusha madai hayo, akisema "ni mwathirika wa mashtaka ya uwongo".
Alilazimika kuchukua likizo kutoka kwa klabu hiyo ili kuwapatia maafisa wa pilosi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo.
Haya yanajiri baada ya miezi mitatu iliyopita , ambapo klabu hiyo iliamua kuwa mchezaji Mason Greenwood hakuwa na mustakabali Old Trafford baada ya tuhuma tofauti za unyanyasaji.
Greenwood, mwenye umri wa miaka 21 alikuwa amekabiliwa na mashtaka ya ubakaji, pamoja na kushambulia. Lakini kesi yake ilitupiliwa mbali baada ya mashahidi wakuu kwenye kesi hiyo kujiondoa na ushahidi mwingine mpya kujitokeza.
Kukosekana kwa Antony na Greenwood aliyejiunga na klabu ya Getafe, kungemfungulia mlango Jadon Sancho hatimaye kufikia bei yake ya pauni milioni 73.
Lakini winga huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ameagizwa kufanya mazoezi peke yake kwa ajili ya kuchuana hadharani na Ten Hag kabla ya mapumziko ya kimataifa baada ya kuachwa nje ya kikosi chake walipopoteza 3-1 dhidi ya Arsenal.
Mholanzi huyo alitaja uchezaji mdogo wa Sancho mazoezini kwa kutocheza, lakini mchezaji huyo alijibu kwamba alikuwa ameitwa "mbuzi wa kuadhibu kwa muda mrefu".