Mustakabali wa winga Jadon Sancho katika klabu ya Manchester United umesalia katika njia panda baada ya klabu hiyo kutoa taarifa kwamba Sancho hatokuwepo katika kikosi cha kwanza cha timu msimu huu.
Fowadi huyo amekuwa katikati ya ugomvi wa umma na meneja Erik ten Hag.
Kocha huyo wa Man United alifichua kwamba Sancho aliondolewa kwenye kikosi dhidi ya Arsenal kutokana na maadili yake ya kazi.
Hata hivyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alijibu kupitia mitandao ya kijamii, akidai kuwa kile alichosema Ten Hag kuhusu yeye si ukweli.
Wawili hao wameshindwa kurekebisha uhusiano wao na Sancho ameondolewa kwenye kikosi.
Sasa atafanya mazoezi tofauti na wachezaji wengine wa kikosi. United wanadai kuwa atarejea kufuatia utatuzi wa suala la nidhamu ya kikosi.
“Jadon Sancho atasalia kwenye programu ya mazoezi ya kibinafsi mbali na kundi la kikosi cha kwanza, akisubiri kusuluhishwa kwa suala la nidhamu ya kikosi,” taarifa fupi iliyoachiliwa kupitia tovuti ya timu ilisoma.
Timu ya Machester United katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wamekuwa wakijipata katika mgogoro na baadhi ya wachezaji wao.
Itakumbukwa mwezi Novemba mwaka jana, aliyekuwa mchezaji wao nguli, Christiano Ronaldo katka mahojiano ya kulipuka aliyofanya na mwanahabari Piers Morgan alifichua mengi kuhusu klabu hiyo na haswa kuhusu tofauti zake na kocha Ten Hag.
Baadae United walitoa taarifa kwamba Ronaldo hatokuwa sehemu ya kikosi cha Ten Hag tena kupelekea kuvunjwa kwa mkataba wake.
Mwezi uliopita, United pia ilitoa taarifa ya kufukuzwa kwa kinda wao Mason Greenwood baada ya uchunguzi wa ndani wa miezi kadhaa kufuatia kesi iliyokuwa inamuandama Greenwood ya unyanyasaji wa kinyumbani.
Kando na hapo, pia hivi majuzi wametangaza kumweka pembeni winga Antony kufuatia madai ya kesi kama hiyo ya unyanyasaji kwa mrembo aliyejitoa akisema kuwa waliwahi kuwa wapenzi na Antony aliwahi kumdhulumu.