Onana aomba kuongea na wanahabari baada ya kufungwa bao la 14 katika mechi ya 6

"Nina mengi ya kuthibitisha, kwa sababu kusema ukweli mwanzo wangu Man United sio mzuri sana" alisema. "Ni mimi niliyeiangusha timu" aliongeza.

Muhtasari

• Katika mechi sita kwenye mashindano yote ambayo Onana ameanza langoni, amefungwa jumla ya mabao 14 huku United wakifanikiwa kufunga mabao 9 tu.

Andre Onana.
Andre Onana.
Image: Facebook

Baada ya Bayern Munich kuwachachafya na kuwatitiga kibano cha mabao 4-3 usiku wa Jumatano, mlinda lango wa timu ya Manchester United Andre Onana aliomba kuzungumza na wanahabari.

Onana ambaye alionekana kufanya makosa mara kwa mara katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza kwenye makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, baada ya kukamilika kwa mechi alitoa ombi la kutaka kufanya mazungumzo na waandishi wa habari za michezo.

Alikiri kwamba yalikuwa ni makosa yake kusababishia timu yake kufungwa, akisema kuwa pasi na makosa yake, pengine wangeshinda maana katika kipindi cha pili walicheza vizuri na nusra warudi mchezoni lakini wakalemewa dakika za zima taa tulale.

“Ni makosa yang utu nakubali, baada ya yale makosa, tulipoteza udhibiti wa mchezo. Ni mimi niliangusha timu yetu kwa kweli. Ni jukumu lango na naubeba msalaba huo  kwa sababu yangu, hatukuweza kushinda. Na sharti nijifunze kutoka kwa makosa hayo kwa ajili ya sasa na baadae,” Onana alisema kwa kujuta.

"Nina mengi ya kuthibitisha, kwa sababu kusema ukweli mwanzo wangu Man United sio mzuri sana".

"Ni mimi niliyeiangusha timu" aliongeza.

Tangu kuanza kwa msimu huu, timu ya Manchester United haijaanza vyema huku safu yao ya nyuma ikitoboka mara kwa mara – jambo ambalo kocha Erik Ten Hag alisema kuwa ni kutokana na kuandamwa kwa majeraha kwa mabeki wake akiwemo Verane, Liandro, Maguire, Shaw na wengine.

Katika mechi sita kwenye mashindano yote ambayo Onana ameanza langoni, amefungwa jumla ya mabao 14 huku United wakifanikiwa kufunga mabao 9 tu.

Aidha, hiki kilikuwa ni kipigo cha 4 kwenye mashindano yote msimu huu.