Sababu ya Sancho kuchelewa mazoezini hadi kutofautiana na kocha ten Hag yafichuka

Nidhamu ya winga huyo ilikuwa shida kila wakati hata wakati alipokuwa Borrusia Dortmund.

Muhtasari

•Sancho kwa kawaida huwa hapati usingizi wa kutosha kutokana na kucheza michezo ya kompyuta usiku kucha hadi asubuhi.

•Sancho alichelewa kufika kwa mazoezi hata akiwa Dortmund kwani alidaiwa kukaa usiku kucha kwenye kompyuta yake akicheza michezo.

Jadon Sancho
Jadon Sancho
Image: X

Imeibuka kuwa winga wa Manchester United, Jadon Sancho ana tatizo la kufika mazoezini kwa kuchelewa, tatizo ambalo linadaiwa kusababishwa na mtindo wake mbaya wa kulala.

Taarifa kutoka Ulaya zinasema kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 23 kwa kawaida huwa hapati usingizi wa kutosha kutokana na tabia yake ya kucheza michezo ya kompyuta usiku kucha hadi asubuhi.

Jarida la Ujerumani BILD limeripoti kuwa tabia hiyo ni moja ya sababu inayoifanya klabu yake ya zamani ya Borrusia Dortmund kuwa na wasiwasi wa kumsaini tena licha ya kuwa ametofautiana wazi na klabu yake ya sasa ya Manchester United. Kulingana na jarida hilo, nidhamu ya winga huyo ilikuwa shida kila wakati hata wakati alipokuwa katika klabu hiyo ya Ujerumani.

"Wakati mwingine alichelewa kufanya mazoezi au aliondoka kwa siku 2 hadi 3 baada ya mechi .. Tatizo kuu lilikuwa kwamba hakuwa akilala vya kutosha kutokana na kucheza mchezo wake wa kompyuta hadi asubuhi," BILD iliripoti.

Inasemekana kwamba Sancho alichelewa kufika kwa mazoezi hata akiwa Dortmund kwani alidaiwa kukaa usiku kucha kwenye kompyuta yake akicheza michezo.

Wakati alipoulizwa kama anafahamu kuhusu uraibu wa Sancho wa kucheza michezo ya kompyuta mapema wiki hii, kocha wa Manchester United Erik ten Hag alisema "Ni juu yake."

"Sizungumzi kuhusu masuala ya kibinafsi na sizungumzi kuhusu wachezaji ambao hawapatikani," ten Haag alisema siku ya Jumanne.

Sancho kwa sasa hayuko kwenye mahusiano mazuri na klabu yake ya Manchester United huku kocha ten Haag awali akimweka kando kwa madai ya kutofanya vyema mazoezini.

Uhusiano mbaya na klabu hiyo ya Uingereza uliongezeka baada ya winga huyo mwenye umri wa miaka 23 kuchagua kujibu madai ya  tena Hag kupitia Twitter ambapo alionekana kupingana naye na baadaye kukataa kuomba msamaha alipotakiwa kufanya hivyo.