Mudryk hatimaye avunja laana, afunga bao la kwanza akiwa Chelsea baada ya kucheza mechi 23

Mudryk alikuwa ameichezea Chelsea jumla ya mechi 23 na akajaribu kufunga mara 26 kabla ya hatimaye kufunga.

Muhtasari

•Mudryk alikuwa amecheza mechi 23 katika mashindano yote akiwa na Chelsea bila kufunga bao hata moja.

•Chelsea ilipata ushindi wa pili katika msimu huu wa EPL 2022/23 na kuwafanya wapande hadi nafasi ya 11 kwenye jedwali wakiwa na pointi 8.

Image: INSTAGRAM// MYKHAILO MUDRYK

Winga wa Chelsea Mykhailo Mudryk alilala mtu mwenye furaha baada ya kufunga bao lake la kwanza akiwa na klabu hiyo baada ya kuhama kutoka Shakhtar Donetsk mwezi Januari mwaka huu.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ukraine mwenye umri wa miaka 22 alikuwa amecheza mechi 23 katika mashindano yote akiwa na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza bila kufunga bao hata moja, jambo lililowafanya mashabiki wa klabu pinzani kumkejeli.

Walakini, laana ya Mudryk ya kutofunga mabao ilimalizika siku ya Jumatatu jioni wakati winga huyo alipoweka bao nyuma ya kipa wa Fulham, Bernd Leno katika dakika ya 18. Raia huyo wa Ukraine alifunga kwa kumalizia pasi nzuri ya beki wa kulia Levi Colwill. Aliugusa mpira kwa kifua chake kabla ya kumaliza kwa urahisi na hatimaye kufunga.

Sekunde chache baada ya Mudryk kufunga, mshambuliaji wa Chelsea, Armando Broja pia alifunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo kwa muda mrefu baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha baya lililomweka nje ya kikosi kwa muda mrefu.

Mudryk ambaye mara nyingi hucheza kama winga wa kulia alifunga katika mechi yake ya 24 akiwa na Chelsea na baada ya kufanya takriban majaribio 26 ya kufunga. Klabu hiyo ilimnunua kwa pauni milioni 88 mwezi Januari, ikipokonya dili la kumsajili kutoka Arsenal ambao walikuwa wakimtafuta kwa muda mrefu.

Mabao hayo mawili, la mchezaji huyo wa Ukraine na Broja yameipa Chelsea ushindi wa pili katika msimu huu wa EPL 2022/23 na kuwafanya wapande hadi nafasi ya 11 kwenye jedwali la Ligi Kuu wakiwa na pointi 8. Kabla ya jana, The Blues walikuwa wameshinda tu dhidi ya Luton Town FC uwanjani Stamford Bridge mwezi Agosti, ikitoka sare mara mbili na kushindwa mara tatu katika EPL msimu wa 2023/24.

Ni vyema kufahamu, washindi hao wa Ligi ya Mabingwa wa 2020/21 walishindwa kufunga bao hata moja kwenye Ligi Kuu mwezi wa Septemba.