Kiungo wa Juventus Nicolo Fagioli apigwa marufuku miezi 7 kwa kukiri kufanya betting

Marufuku hiyo inakuja kama pigo kubwa kwa Juventus huku miamba hao wa Serie A wakipoteza kiungo mwingine baada ya Paul Pogba.

Muhtasari

• Adhabu ya kusimamishwa kwa miezi 12 ilitolewa Jumanne, ingawa miezi mitano kati ya hiyo itatolewa kwa njia mbadala.

Nicolo Fagioli
Nicolo Fagioli
Image: Facebook

Kiungo wa Juventus Nicolo Fagioli amepigwa marufuku ya miezi saba kutojihusisha na soka kwa kosa la kuweka kamari kwenye majukwaa yasiyo halali.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia hatacheza tena msimu huu baada ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa Turin kumpa marufuku ya miezi saba kutojihusisha na soka kwa kuweka dau kwenye majukwaa yasiyo halali.

Adhabu ya kusimamishwa kwa miezi 12 ilitolewa Jumanne, ingawa miezi mitano kati ya hiyo itatolewa kwa njia mbadala.

Fagioli pia amepigwa faini ya $13,000, sawa na shilingi za Kenya milioni 2 na pia atahitajika kuhudhuria marekebisho ya kuondokana na uraibu wa Kamari.

Kusimamishwa huku ni punguzo kubwa la adhabu ambayo hutolewa kwa ujumla kwa ukiukaji wa Kifungu cha 24 cha Kanuni ya Haki ya Michezo, ambayo ni miaka mitatu, huku uamuzi wa mwisho ukitolewa kwa msingi wa mashauriano ya kesi na mawakili wa Fagioli.

Sababu kuu ya kupunguzwa kwa adhabu ni kwa sababu ya ushirikiano kamili wa mchezaji na mahakama na hamu yake ya kupambana na uraibu wa kucheza kamari.

Hata hivyo, marufuku hiyo inakuja kama pigo kubwa kwa Juventus huku miamba hao wa Serie A wakipoteza kiungo mwingine baada ya Paul Pogba, ambaye anakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa muda mrefu kwa kukutwa na dawa zilizopigwa marufuku.

Vijana wa Massimiliano Allegri watamenyana na AC Milan katika mchuano wa Serie A Jumapili.