Alikiba kutumbuiza kwenye sherehe za ufunguzi wa African Football League

Mataifa 8 ya Afrika yalipata nafasi murwa ya kutoa timu 8 ambazo zitashiriki kwenye kinyang’anyiro hicho.

Muhtasari

• Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Simba SC wakiwa kama mwenyewe wa mashindano hayo dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

• Shindano hilo la kipekee lilizinduliwa mwaka jana likiwa na dau ya zawadi la dola milioni 4 kwa washindi.

Alikiba kutumbuiza AFL
Alikiba kutumbuiza AFL
Image: X

Msanii wa kizazi kipya wa muda mrefu kutokea nchini Tanzania, Alikiba amethibitisha kuwa atakuwepo kama mmoja wa wasanii watakaotumbuiza kwenye sherehe za ufunguzi wa shindano la African Football League.

Shindano hilo linazinduliwa leo Ijumaa, Oktoba 20 katika uwanja wa kimataifa wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na linajumuisha vilabu wa mpira pendwa wa miguu kutoka mataifa 8 kote Afrika.

Ikiwa ni siku ya kwanza kwa mashindano hayo, kama kawaida kutakuwepo na sherehe za ufunguzi ambazo Alikiba kupitia ukurasa wake wa X, awali ukijulikana kama Twitter amethibitisha kutia nakshi kwenye nyuso za mashabiki wake.

“Sherehe za Kufungua ligi ya mpira wa miguu Afrika… Tukutane Ijumaa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa,” Alikiba aliandika mapema Alhamisi huku akipakia picha za mara ya mwisho akitumbuiza katika uwanja huo mwezi Agosti wakati wa Simba Day – siku ya klabu ya Simba SC kusherehekea ufunguzi wa msimu mpya na mashabiki wake.

Mataifa 8 ya Afrika yalipata nafasi murwa ya kutoa timu 8 ambazo zitashiriki kwenye kinyang’anyiro hicho.

Timu hizo 8 zitakuwa ni Simba SC kutoka taifa la Tanzania, Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini, Petro Atletico de Luanda kutoka Angola, TP Mazembe ya DRC, Esperance ya Tunisia, Al Ahly ya Misri, Enyimba ya Nigeria na Wydad ya Morocco.

Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Simba SC wakiwa kama mwenyewe wa mashindano hayo dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

Shindano hilo la kipekee lilizinduliwa mwaka jana likiwa na dau ya zawadi la dola milioni 4 kwa washindi.

Taarifa amabzo hata hivyo hazijathibitishwa zinaakisi kwamba rais wa FIFA Gianni Infantino na aliyekuwa mkufunzi wa muda mrefu wa Arsenal ya Uingereza, Arsene Wengr ni miongoni mwa majina makubwa watakaoshuhudia ufunguzi wa kinyang’anyiro hicho.