logo

NOW ON AIR

Listen in Live

African Football League: Simba S.C, Atletico watimuliwa kwenye Ligi ya Soka ya Afrika

Simba imetimuliwa kutoka mashindano ya AFL baada ya mechi ya mkondo wa pili na Al Ahly ya Misri ambayo iliishia sare ya 1-1.

image
na Samuel Maina

Michezo25 October 2023 - 04:22

Muhtasari


  • •Simba S.C imetimuliwa kutoka mashindano ya AFL baada ya mechi ya mkondo wa pili na Al Ahly ya Misri ambayo iliishia sare ya 1-1. 
  • •Timu ya pili iliyotoka kwenye kinyang'anyiro hicho Jumanne ni Petro Atletico ya Angola ambayo ilitoka sare ya 0-0 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
aliwafungia Simba ila wakakosa kufuzu kwa nusu fainali.

Mechi mbili za kwanza za mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) zilichezwa siku ya Jumanne jioni.

Simba S.C ya nchi jirani ya Tanzania imetimuliwa kutoka mashindano hayo baada ya mechi ya mkondo wa pili na Al Ahly ya Misri ambayo iliishia sare ya 1-1. Mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, mjini Cairo, Misri mwendo wa saa kumi na moja jioni Jumanne.

Simba S.C ambao walikuwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele na kuiwakilisha Afrika Mashariki katika hatua ya nusu fainali walitangulia kupata bao kupitia kwa Sadio Kanoute katika dakika ya 68 kabla ya Kahraba kuifungia Al Ahly bao zuri katika dakika ya 76. Hakuna mabao zaidi yaliyoshuhudiwa kwenye mechi hiyo ikimaanisha kuwa Al Ahly walikuwa wamefuzu hatua inayofuata kwa sababu ya mabao mengi ya ugenini.

Mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2. Reda Slim na Kahraba waliifungia Al Ahly huku mabao ya Simba S.C yakifungwa na Denis Kibu na Sadio Kanoute.

Timu ya pili iliyotoka kwenye kinyang'anyiro hicho Jumanne ni Petro Atletico ya Angola ambayo ilitoka sare ya 0-0 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Petro Atletico walikuwa wamepoteza kwa Mamelodi 0-2 nyumbani wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza wiki iliyopita ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro mjini Luanda, Angola.

Mechi zijazo za mkondo wa pili zitachezwa siku ya Alhamisi ambapo Esperance Tunis ya Tunisia itavaana na TP Mazembe ya DR Congo. Mazembe wana faida kubwa kwani walimfunga mpinzani wao 1-0 katika uwanja wa nyumbani, Stage TP Mazembe wiki iliyopita.

Wydad ya Morocco itahitaji tu ushindi au sare moja ili kufuzu kwa nusu fainali katika mechi yao ya nyumbani na Enyimba ya Nigeria Alhamisi usiku. Miamba hao wa Morocco waliwashinda wapinzani wao wa Nigeria 0-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa nchini Nigeria wiki iliyopita.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved