Siku ya Alhamisi, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilitoa orodha mpya timu za kimataifa kulingana na jumla ya pointi walizopata.
Katika orodha hiyo mpya iliyochapishwa kwenye tovuti ya shirikisho hilo, washindi wa kombe la dunia la mwaka wa 2022, Argentina wamechukua nafasi ya kwanza kwa jumla ya pointi 1861.29 huku washindi wa awali wa Kombe la Dunia, Ufaransa wakishika nafasi ya pili kwa jumla ya pointi 1853.11.
Brazil inachukua nafasi ya tatu kwa jumla ya pointi 1812.2 huku Uingereza ikichukua nafasi ya nne ikiwa na jumla ya pointi 1807.88. Ubelgiji inafunga orodha ya tano bora kwa jumla ya alama 1793.71.
Timu bora ya Afrika ni Morocco ambayo imeorodheshwa katika nambari 13 katika orodha ya FIFA ikiwa imevuna pointi 1658.49. Senegal ambayo ni timu ya pili bora Afrika imeorodheshwa ya 20 duniani ikiwa na pointi 1600.82 ikifuatiwa na Tunisia ambayo imeshika nafasi ya 32 duniani kwa pointi 1516.14.
Timu nyingine za Afrika zilizoingia kwenye orodha ya 100 bora duniani ni pamoja na Algeria (33), Misri (35), Nigeria (40), Cameroon (43), Mali (47), Cote d'Ivoire (52), Burkina Faso (56). , Ghana (60), Afrika Kusini (64), DRC Congo (65), Cape Verde (74), Guinea (80), Zambia (81), Gabon (86), Uganda (90), Equatorial Guinea (91) na Benin (93).
Harambee Stars ya Kenya imeshuka nafasi moja hadi nambari 110 ikiwa na pointi 1186.85 huku nchi jirani ya Tanzania ikichukua nafasi ya 121 ikiwa na pointi 1146.46. Barani Afrika, Kenya imeorodheshwa nambari 24 kati ya nchi 54.
Rwanda inashika nafasi ya 140 ikiwa na pointi 1087.03 huku jirani wake Burundi ikifuata katika nambari 141 kwa pointi 1080.43.