Benzema ashinda katika mzozo wake na Kocha Nuno Espirito Santos klabuni Al Ittihad

Benzema na kocha wake Nuno wamekuwa wakitofautiana kwa muda sasa tangu aliposajiliwa na timu hiyo na mzozo wao ulifikia kilele Jumatatu baada ya kichapo kwenye ligi ya mabingwa AFC.

Muhtasari

• Meneja huyo mzoefu wa Ureno aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 14 mwezi Mei.

• Sasa bila meneja, ripoti zinaonyesha kuwa Al-Ittihad inaweza kujaribu kuajiri Mfaransa ili kumfurahisha Benzema.

Benzemac ataja sababu ya kukubali mkataba mnono wa Al Itihad
Benzemac ataja sababu ya kukubali mkataba mnono wa Al Itihad
Image: Instagram

Klabu ya Al Ittihad inayoshiriki katika ligi kuu ya Saudi Pro League, imefikia hatima ya kumfuta kazi kocha Nuno Espirito Santos kufuatia mzozo wa miezi kadhaa na mshambuliaji wake aliyesajiliwa msimu wa majira ya joto kwa dau kubwa, Karim Benzema.

Inaarifiwa kwamba Santos aliotesha kibarua chake nyasi Jumanne, Novemba 7 ikiwa ni siku moja tu baada ya kupapurana hadharani na Benzema.

Nuno na nyota huyo wa zamani wa Real Madrid walijibizana vikali kufuatia kichapo cha 2-0 cha klabu hiyo kutoka kwa Al Quwa Al Jawiya ya Iraq kwenye Ligi ya Mabingwa ya AFC siku ya Jumatatu.

Kulingana na jarisa la GOAL, matokeo hayo yalizua ugomvi mkali wa maneno kati ya nahodha na meneja, huku Benzema na Nuno wakionekana kutupiana matusi kwa muda baada ya kipenga cha mwisho.

Al-Ittihad hawajashinda katika mechi zao tano za mwisho kwenye Ligi ya Saudi Pro, na kipigo dhidi ya Al Quwa Al Jawiya kilikuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la wamiliki wa kilabu, ambao walilazimika kufanya uamuzi.

Sasa bila meneja, ripoti zinaonyesha kuwa Al-Ittihad inaweza kujaribu kuajiri Mfaransa ili kumfurahisha Benzema, ambaye bado hajafikia kilele cha talanta yake na klabu ya Saudi, Sports Brief walifichua.

Wakati huo huo, licha ya uwekezaji mkubwa kwa wachezaji kama vile Karim Benzema na Ngolo Kante msimu wa joto, Nuno Espirito Santo alisimamia ushindi mara mbili pekee katika michezo tisa iliyopita ya Al-ttihad katika mashindano yote, Daily Mirror inaripoti.

Meneja huyo mzoefu wa Ureno aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 14 mwezi Mei, akiwa tayari ameshinda Kombe la Saudia Super Cup, lakini mwanzo mbaya wa kampeni za msimu huu ulimfanya aondoke.