AFL: Mamelodi Sundowns yapiga Wydad 2-0 na kushinda Kombe la Ligi ya Soka ya Afrika

Sundowns watapata Ksh 600.32m kufuatia ushindi huo huku Wydad wakiaondoka na Ksh 450.24m kwa kuibuka wa pili.

Muhtasari

•Mamelodi Sundowns imeibuka klabu ya kwanza kabisa kushinda taji la Ligi ya Soka ya Afrika iliyoanzishwa hivi majuzi.

•Sundowns walichukua uongozi kupitia kwa  Peter Shalulile kabla ya Aubrey Modhiba kuwapa bao la pili.

wameibuka washindi wa African Football League
Mamelodi Sundowns wameibuka washindi wa African Football League
Image: HISANI

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imeibuka klabu ya kwanza kabisa kushinda taji la Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) iliyoanzishwa hivi majuzi.

Sundowns walitawazwa washindi wa taji hilo kubwa la Afrika siku ya Jumapili jioni baada ya kuifunga Wydad Casablanca ya Morocco 2-0 katika mechi ya mkondo wa pili wa fainali iliyochezwa nyumbani kwao Pretoria, Afrika Kusini. Mechi hiyo ya kufana ilichezwa katika uwanja wa Loftus Versfeld.

Ushindi huo uliwapa wababe hao wa soka wa Afrika Kusini jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliochezwa jijini Casablanca, Morocco siku saba zilizopita.

Sundowns walichukua uongozi kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza cha mechi kupitia kwa  Peter Shalulile kabla ya Aubrey Modhiba kuwapa bao la pili takriban dakika saba baada ya kipindi cha pili kuanza.

Rais wa FIFA Gianni Infantino alikuwa miongoni mwa waliohudhuria mechi ya fainali mjini Pretoria siku ya Jumapili, pamoja na umati mkubwa wa mashabiki ambao walikuwa wameruhusiwa kuingia bure.

Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) ilitangazwa na rais wa FIFA, Gianni Infantino mwaka wa 2019 na ikazinduliwa mara ya kwanza na CAF mnamo Agosti 10, 2022.

Msimu wa kwanza kabisa wa ligi hiyo maalum ya Afrika ulianza rasmi Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Rais wa FIFA, Gianni Infantino na kocha wa zamani, Arsene Wenger walikuwepo mnamo siku ya ufunguzi.

AFL ilipangwa kujumuisha vilabu 24, lakini Shirikisho la Soka ya Afrika (CAF)  likapunguza hadi 8 kwa msimu wa kwanza.

Timu zilizoshiriki zilichaguliwa kutoka kwa ligi 8 bora barani Afrika na zote zilikuwa uhakika wa kutunzwa Ksh 150m.

Timu zilizotinga nusu fainali zitazawadiwa Ksh 255.1m huku timu ya pili ikiondoka na Ksh 450.24m na washindi Ksh 600.32m.