Kwa nini viwanja vya Kenya havijai mashabiki- Jacob 'Ghost' aeleza

Ghost alisema kuwa Wakenya hawana uzalendo na hawajivunii kile ambacho taifa linacho.

Muhtasari

•“Wakenya tuko wacheshi sana, mimi nikiwa mmoja wao. Wakenya sisi hatujielewi sisi ni nani, tunataka nini kama Wakenya?,” Ghost alisema.

•Ghost alitoa wito kwa Wakenya kubadili mawazo yao na kuanza kujivunia kile tulichonacho ili kukikuza.

Aliyekuwa kocha wa Harambee Stars, Jacob 'Ghost' Mulee

Kocha wa zamani wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee ameeleza ni kwa nini soka la Kenya halishabikiwi kama ilivyo katika mataifa mengine, k.v Tanzania.

Akizungumza kwenye mahojiano na mchekeshaji Chipukeezy kwenye kipindi cha Chipukeezy Show, Ghost alisema kuwa Wakenya hawana uzalendo na hawajivunii kile ambacho taifa linacho, jambo ambalo limewafanya kutoshabikia sanaa ya humu nchini kama vile soka na muziki.

“Wakenya tuko watu wacheshi sana, mimi nikiwa mmoja wao. Wakenya sisi hatujielewi sisi ni nani, tunataka nini kama Wakenya?,” Ghost Mulee alisema.

Aliongeza, “Sio soka pekee yake, hata kimuziki. Sisi kama Wakenya, tuna nini? Fahari yetu ni nini? Hatuna uzalendo.”

Kocha huyo ambaye pia ni mtangazaji wa redio alibainisha kuwa Wakenya wengi wanajitambulisha na vilabu vya soka vya Ulaya k.m Manchester United na Arsenal badala ya kusapoti vilabu vyetu vya soka vya humu nchini.

“Unapata mtu anasema, ‘mimi ni Man U damu!’, wewe damu ya Man U ulitoa wapi? Ati mimi ni Arsenali!!" Acheni mchezo, tusidanganye,” alisema.

Kufutia hayo, alisema ili soka la Kenya listawi, lazima wananchi wakumbatie tulichonacho na kujivunia.

Ghost alitoa mfano wa jinsi wananchi wa nchi jirani yetu Tanzania wanavyoonyesha upendo na sapoti kwa vilabu vyao vya soka na kuifanya ligi ya Tanzania kuwa miongoni mwa ligi bora zaidi kufuatiliwa barani Afrika.

“Huko, uwanja ikifika saa nane washafunga. Hakuna mtu kuingia. Na mechi inaanza saa kumi. Yaani ukienda Dar es Salaam siku ya derby ya Simba na Yanga, mjini hakuna mtu kwa sababu hiyo ni siku ya derby. Saa nane wamefunga stadium wanatangaza ‘60000 capacity imejaa hakuna mtu mwingine ataingia,” Ghost alisema.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi alifichua kuwa katika mchezo mkubwa nchini Tanzania, jumla ya shilingi milioni 20-30 hukusanywa langoni.

"Sababu kubwa ni kuwa wanapenda timu zao," Ghost alisema.

Ghost alitoa wito kwa Wakenya kubadili mawazo yao na kuanza kujivunia kile tulichonacho ili kukikuza.