Balotelli adai timu ya taifa ya Italy haijapata straika mahiri kama yeye, ataka kurejeshwa kikosini

Tangu 2018, amepitia vilabu mbalimbali vikiwemo Nice, Marseille, Brescia, Monza na kwa sasa yuko katika muhula wake wa pili na Uturuki, timu ya daraja la juu Adana Demirspor.

Muhtasari

• "Ikiwa niko mzima, bado ninajiona kuwa mwenye nguvu zaidi." Balotelli alisema.

Mario Balotelli
Mario Balotelli
Image: Facebook

Mchezaji wa zamani wa Manchester City na Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Mario Balotelli ameelezea hamu yake ya kurejea katika timu ya taifa ya Italia, akisisitiza imani yake kuwa chaguo kubwa zaidi kati ya washambuliaji wa sasa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, ambaye hayupo kwenye kikosi cha Azzurri tangu sare ya 1-1 dhidi ya Poland Septemba 2018, amepitia vilabu mbalimbali vikiwemo Nice, Marseille, Brescia, Monza na kwa sasa yuko katika muhula wake wa pili na Uturuki, timu ya daraja la juu Adana Demirspor.

Balotelli, aliyesherehekewa kwa jukumu lake kuu katika ushindi wa nusu fainali ya Euro 2012 ya Italia dhidi ya Ujerumani, alielezea hisia zake baada ya Italia kufuzu kwa michuano ijayo ya Ulaya chini ya uongozi wa kocha mpya Luciano Spalletti.

Mshambulizi huyo, akiwa na shauku ya kuthibitisha msimamo wake katika masuala ya uteuzi wa timu ya taifa, alitoa maoni yake kuhusu uchezaji wa wachezaji wengine wa mbele hivi karibuni, akisema, "Ikiwa niko mzima, bado ninajiona kuwa mwenye nguvu zaidi."

Katika mahojiano yake na TvPlay kupitia Calciomercato.com, Balotelli alitilia shaka mchango wa Giacomo Raspadori na Gianluca Scamacca katika mechi ya hivi majuzi, akionyesha ukosefu wa matokeo ya kuridhisha.

"Ikiwa niko mzima, bado ninajiona kuwa mwenye nguvu zaidi. Je, [Giacomo] Raspadori na [Gianluca] Scamacca walicheza jana? Je, walipiga shots ngapi kwa pamoja? Mbili? Nataka kupona na kuchezea timu ya taifa.”

"Siku zote natumai wito. Nilikutana na Spalletti na nimekutana naye mara kadhaa. Tulifanya mzaha tulipokutana kwenye mechi ya kirafiki na Napoli, lakini sina uhusiano.”