Erik Ten Hag awaomba wamiliki wa Man Utd kumpa muda zaidi kusuka kikosi na wasimfute

Timu hiyo iko mkiani mwa kundi lao la Ligi ya Mabingwa ikiwa imesalia na mchezo mmoja, ikikabiliwa na hatari ya kuondolewa, na tayari imetupwa nje ya Kombe la Carabao.

Muhtasari

• Ten Hag alikuwa na msimu mzuri wa kwanza akiwa na Manchester United, na kuwaongoza kutwaa taji lao la kwanza baada ya miaka sita.

• Hata hivyo, msimu wake wa pili umekumbwa na misukosuko, na kibarua chake kimeanza kuchunguzwa.

Erik Ten Hag
Erik Ten Hag
Image: Manchester United

 Baada ya majarida kadhaa ya spoti nchini Uingereza kuripoti Jumanne kwamba kocha Erik Ten Hag wa Manchester United amepoteza uunaji mkono katika nusu ya chumba cha kubadilisha nguo, ripoti hizo zilikanushwa na klabu lakini sasa Ten Hag ameomba uongozi wa timu hiyo kumpa muda Zaidi wa kusuka kikosi na wasimfute.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari baada ya vyombo vingine kadhaa kufungiwa kuhudhuria mazungumzo yake mbele ya mtanange mkali dhidi ya Chelsea usiku wa Jumatano, Ten Hag aliwataka wamiliki wa klabu kuwa na Imani naye, akisisitiza kwamba yeye ndiye mkufunzi faafu kwa klabu hiyo yenye msukosuko kwa Zaidi ya miaka 10 tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

"Siku zote kutakuwa na nyakati ngumu katika kila safari. Tunaelekea kwenye njia sahihi. Najua tutafika pale tunapotaka. Angalia rekodi yangu. Kila mahali nimekuwa, kila msimu, nimefikia malengo yangu. Kwa hiyo, tukishikamana, tushikamane na mpango na mkakati, tutafika tunapotaka,” Ten Hag alisisitiza.

Manchester United kwa sasa inashika nafasi ya saba kwenye jedwali la Premier League ikiwa na pointi 24 baada ya mechi 14 za mwanzo, ikiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo Arsenal kwa pointi 12 (ingawa Arsenal imecheza mchezo mmoja zaidi).

Timu hiyo iko mkiani mwa kundi lao la Ligi ya Mabingwa ikiwa imesalia na mchezo mmoja, ikikabiliwa na hatari ya kuondolewa, na tayari imetupwa nje ya Kombe la Carabao.

Ten Hag alikuwa na msimu mzuri wa kwanza akiwa na Manchester United, na kuwaongoza kutwaa taji lao la kwanza baada ya miaka sita. Hata hivyo, msimu wake wa pili umekumbwa na misukosuko, na kibarua chake kimeanza kuchunguzwa.

United imepoteza mechi sita kati ya 14 za mwanzo za Ligi ya Premia, huku kipigo cha 1-0 Jumamosi kutoka kwa Newcastle kikiwa kupoteza kwao kwa 10 katika michezo 21 katika mashindano yote.