Olunga, Namwamba wavunja kimya baada ya nyota wa Junior Stars kuzimwa na Uganda

Olunga alisema anajivunia wanasoka hao chipukizi na akabainisha kuwa mustakabali wa soka la Kenya ni mzuri.

Muhtasari

•Olunga ameipongeza timu ya Kenya ya Vijana kwa matokeo mazuri katika mashindano ya wavulana ya CECAFA U-18.

•Namwamba pia alielezea fahari yake kwa wachezaji chipukizi na kuzungumzia kuhusu mipango ya kujenga soka la Kenya.

Junior Stars
Image: TWITTER// ABABU NAMWAMBA

NAHODHA wa Harambee Stars, Michael Olunga Ogada ameipongeza timu ya Kenya ya Vijana walio chini ya umri wa miaka 18 kwa matokeo mazuri katika mashindano ya wavulana ya CECAFA U-18.

Junior Stars waliibuka wa pili kwenye mashindano hayo yaliyokamilika Ijumaa, Desemba 8 baada ya kulazwa 1-2 na timu ya vijana ya Uganda U-18 wakati wa mechi ya fainali ambayo ilichezwa katika Uwanja wa Jomo Kenyatta Mamboleo mjini Kisumu. Walikuwa wamefuzu kwa fainali hizo baada ya kufanya vyema katika mashindano hayo na baada ya kuifunga timu ya U-18 ya Tanzania katika nusu fainali.

Huku akiipongeza timu hiyo ya vijana Ijumaa alasiri, Olunga alisema anajivunia wanasoka hao chipukizi na akabainisha kuwa mustakabali wa soka la Kenya ni mzuri.

"Ninajivunia juhudi za pamoja za timu ambayo timu hii imeweka. Mustakabali ni mzuri. Bahati ngumu. Nchi mbele,” Olunga alisema kupitia Twitter.

Waziri wa michezo na sanaa, Bw Ababu Namwamba pia alielezea fahari yake kwa wachezaji chipukizi na kuzungumzia kuhusu mipango ya kujenga soka la Kenya.

“Big up boys. Ninajivunia nyinyi sana. Huu ni mwanzo tu tunapojenga siku za usoni kwa umakini wa makusudi, wa mpango na muundo,” alisema.

Uganda walitawazwa mabingwa wa Cecafa U18 2023, baada ya kutoka nyuma na kuwapiga wenyeji Kenya 2-1 katika mchuano mkali wa fainali katika uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu Ijumaa.

Syphas Owuor aliifungia Kenya bao la kuongoza baada ya kupita walinzi na kufunga na kupelekea umati wa mashabiki kusherehekea kwa shangwe katika dakika ya 66.

Hata hivyo, Richard Okello aliharibu karamu ya Kenya baada ya kutumia nafasi kwenye ukingo wa eneo la hatari katika dakika ya 78, na kulazimisha pambano hilo hadi muda wa ziada.

Hakim Mutebi alikuwa chachu kwa wageni, akifunga wavu kwa sekunde 50 tu baada ya muda wa ziada na kuwapatia kbao muhimu lililowatenganisha mabeberu hao wawili wa Afrika Mashariki kwenye kipyenga cha muda wote.