Sadio Mane azindua uwanjani alioujenga kwa gharama zake mwenyewe kijijini mwao

"Nimefurahi sana kuwa nanyi leo na kuwakaribisha nyumbani kwangu, katika kijiji changu cha asili cha Bambali, ambapo yote yalianzia," alisema

Muhtasari

• Mbali na uwanja huo, Mane amechangia hapo awali maendeleo ya shule kadhaa, hospitali, na rasilimali muhimu nchini Senegal.

Sadio Mane azindua uwanja.
Sadio Mane azindua uwanja.
Image: X

Mcheza kandanda wa Senegal, Sadio Mane, anayesifika kwa kazi yake nzuri akiwa na Liverpool na kwa sasa anachezea klabu ya Al-Nasr ya Saudia, ameonyesha nia yake ya kuleta maendeleo ya jamii kwa kuzindua uwanja mpya kabisa katika kijiji alichozaliwa cha Bambali.

Kwa mujibu wa video na picha ambazo zimeenezwa katika mitandao ya kijamii, Uwanja huo mdogo, unaofadhiliwa kabisa na Mane mwenyewe, unachukua nafasi ya uwanja wa matope ambapo mshambuliaji huyo mwenye kipawa alionekana akicheza miaka miwili tu iliyopita wakati wa ziara ya nje ya msimu nchini Senegal.

Jengo jipya lililojengwa hivi karibuni, ambalo sasa limepewa jina rasmi la Stade De Bambali, lilizinduliwa katika sherehe kubwa ya ufunguzi iliyohudhuriwa na watu mashuhuri kutoka taifa la Senegal.

Tukio hilo lilitumika kama fursa kwa jamii kutoa shukrani na kuunga mkono mpango wa ajabu wa Mane kuelekea mahali alipozaliwa.

"Nimefurahi sana kuwa nanyi leo na kuwakaribisha nyumbani kwangu, katika kijiji changu cha asili cha Bambali, ambapo yote yalianzia," alisema, kama alivyonukuliwa na Wiw Sport.

Mnamo 2022, Mane alicheza mechi kwenye uwanja wa asili wa matope kabla ya kuamua kuubadilisha kuwa uwanja wa kisasa kwa gharama yake mwenyewe.

Ukarimu wa Sadio Mane umemfanya ashangiliwe sana katika bara zima, akionyesha kujitolea kwake kutoa uhisani zaidi ya uwanja wa soka.

Mbali na uwanja huo, Mane amechangia hapo awali maendeleo ya shule kadhaa, hospitali, na rasilimali muhimu nchini Senegal.

Wakati huo huo, Mane atakuwa na lengo la kutetea taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) akiwa na Senegal huku wakijiandaa kwa makala ya 2023 ambayo yataanza wiki ijayo nchini Ivory Coast.