Harambee Stars haigopi Brazil au Argentina huku wakilenga kucheza vs Ufaransa na Italia

Ushindi wa Kenya wa 2-1 dhidi ya Qatar na sare ya 2-2 dhidi ya Urusi katika mechi za kirafiki unaweza tu kuhusishwa na uwezo wa Firat wa kuamsha hali ya kujiamini.

Muhtasari

•  Haya ni kwa mujibu wa mkufunzi msaidizi, Ken Odhiambo katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini.

Harambee Stars haiogopi Argentine, Brazil
Harambee Stars haiogopi Argentine, Brazil
Image: Facebook

Mwezi mmoja  baada ya kocha wa Harambee Stars, Engin Firat kudai kwamba yumo mbioni kutafuta mazungumzo na mashirikisho ya soka nchini Ufaransa na Italia kutafuta nafasi ya kushiriki mechi za kirafiki na wababe hao wa Ulaya, sasa anadai haogopi hata timu za mataifa ya Argentina na Brazil.

Haya ni kwa mujibu wa mkufunzi msaidizi, Ken Odhiambo katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini.

Odhimabo alisema kwamba kocha mkuu Engin Firat yuko tayari muda wowote kushiriki mchezo wa kandanda dhidi ya miamba hao wa Amerika ya kusini pasi na kuogopa umahiri wa timu zao za kitaifa kaitka ulingo wa soka.

“Jambo moja kuhusu kocha [Engin Firat] ni kujiamini kwake; haogopi hata Brazil wala Argentina. Walete, naye atawachukua,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Kenya.

Kulingana na kocha mkuu wa zamani wa Bandari na Sofapaka, ushindi wa Kenya wa 2-1 dhidi ya wenyeji wa Kombe la Dunia 2022 Qatar na sare ya 2-2 dhidi ya wenyeji wa Kombe la Dunia 2018 Urusi katika mechi za kirafiki unaweza tu kuhusishwa na uwezo wa Firat wa kuamsha hali ya kujiamini.

Kauli hiyo ya naibu kocha inakuja mwezi mmoja tu baada ya kocha Firat kufichua kwamba anapanga mikakati ya kusaka mechi za kirafiki dhidi ya Ufaransa na Italia katika sku zijazo.

Katika mahojiano na gazeti la People Daily, Firat alisema kwamba wengi huenda wakapuuzilia mbali ndoto hiyo wakisema kuwa ni hekaya za Abunuwasi lakini yeye yuko imara na atasukuma hai ahakikishe ombi lake kwa Italia na Ufaransa limeitikiwa.

“Ninapanga kupata mechi dhidi ya timu kubwa, pengine mabingwa wa zamani wa dunia Ufaransa au Italia. Watu wengine wanaweza kudhani ni ndoto tu, lakini kupitia mawasiliano yangu ya karibu, itafanyika," alisema Firat.