Timu nzima ya Gambia yanusurika kifo wakiwa ndani ya ndege kwenda kipute cha AFCON

Abiria wengi wanasemekana kusinzia muda mfupi baada ya ndege kupaa. Hata hivyo, maafa yalizuiliwa huku ndege hiyo ikirejea Gambia baada ya dakika 20 pekee.

Muhtasari

Kijana wa zamani wa Manchester United Saidy Janko pia alikuwa kwenye ndege hiyo na alichapisha ujumbe mrefu kuhusu tukio hilo.

Timu ya Gambia
Timu ya Gambia
Image: X//TheGambiaFF

Timu ya taifa ya Gambia ilihusika katika tukio la kuogofya kwenye ndege yao kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON, Jumatano jioni.

Imeripotiwa kuwa wachezaji kadhaa walizirai kutokana na kukosa hewa ya oksijeni kwenye ndege.

Abiria wengi wanasemekana kusinzia muda mfupi baada ya ndege kupaa. Hata hivyo, maafa yalizuiliwa huku ndege hiyo ikirejea Gambia baada ya dakika 20 pekee.

Timu ya taifa ya Gambia ni pamoja na nyota wa Wrexham Jacob Mendy.

"Sote tungeweza kuwa tumekufa," kocha Tom Saintfiet anaripotiwa kusema na De Telegraaf. “Sote tulilala haraka. Mimi pia. Nilikuwa na ndoto fupi kuhusu jinsi maisha yangu yalivyofanyika. Kweli na kweli,” Alinukuliwa na talkSPORT.

"Baada ya dakika tisa rubani aliamua kurejea kwa sababu hakukuwa na usambazaji wa oksijeni. Kulikuwa na wachezaji ambao hawakuamka mara baada ya kutua. Karibu tupate sumu ya kaboni monoksidi. Nusu saa nyingine ya kuruka na sote tungekuwa tumekufa."

Kijana wa zamani wa Manchester United Saidy Janko pia alikuwa kwenye ndege hiyo na alichapisha ujumbe mrefu kuhusu tukio hilo.

Aliandika: "Baada ya kusafiri kwa jumla ya saa 32 kutoka Saudi Arabia (Kambi ya Mafunzo) hadi Gambia na mapumziko marefu huko Istanbul na Casablanca, tulipaswa kusafiri kwa ndege kutoka Gambia hadi Ivory Coast kwa AFCON leo.”

"Tulipoingia tu kwenye ndege ndogo iliyokodiwa kuturusha, tuliona joto kali lililotuacha tukitokwa na jasho. Tulihakikishiwa na Wafanyakazi kwamba hali ya hewa ingeanza tukiwa angani.”