Senegal itashinda AFCON kuwaonyesha hatukuenda Saudia kustaafu – kipa Edouard Mendy

Kando na Mendy ambaye yuko Saudi Arabia, wachezaji wenzake waliojiunga naye kwenye ligi hiyo ni pamoja na mshambulizi Sadio Mane anayechezea Al Nassr na Kalidou Koulibaly anayesakatia Al Hilal.

Muhtasari

• "Kiwango cha ligi hii ni cha juu sana na usipofanya vizuri hapa, huwezi kufanya vizuri kwenye timu ya taifa."

Wachezaji wa AFCON.
Wachezaji wa AFCON.
Image: Facebook

Mlinda lango wa timu ya Al Ahli ya nchini Saudi Arabia ambaye pia ni kipa nambari moja wa timu ya taifa ya Senegal, Edouard Mendy ameonesha Imani yake kuwa taifa hilo litatetea taji lao la AFCON katika Makala ya mwaka huu nchini Ivory Coast.

Akizungumza huko nchini Saudi Arabia muda mchache baada ya kuondoka kujiunga na timu ya Senegal nchini Ivory Coast kwa kipute cha AFCON, Mendy alisema kuwa wachezaji wenza katika timu ya taifa walioshinda naye AFCON mwaka juzi wamejiunga na ligi ya Saudi Pro League.

Mendy alisema kuwa wamekuwa wakisemwa kuwa walijiunga na ligi ya Saudia kama njia moja ya kustaafu lakini safari hii wanakwenda kulitetea taji hilo kama ishara ya kuthibitisha kuwa hawakuenda Saudi kustaafu.

"Tumekuwa tukizungumza kuhusu Kombe la Afrika tangu tuliposajiliwa kwa sababu bila shaka tulishinda la mwisho hivyo tunataka kufanya michuano bora zaidi Januari, niliwahi kuzungumza na Sadio na Kalidou kuhusu hilo, bila shaka, tuna jukumu kubwa, sisi ndio viongozi katika timu hii," aliambia vyombo vya habari vya Saudi Pro League.

“Tunaambiana sisi tupo hapa (Saudi Arabia) lakini hatuwezi kuwa wabaya, haiwezekani, tunatakiwa kuwa bora zaidi ya sisi wenyewe. Hatukuja hapa kwa ajili ya kustaafu kama watu wengine wanasema. Ni makosa kabisa," aliongeza.

Kando na Mendy ambaye yuko Saudi Arabia, wachezaji wenzake waliojiunga naye kwenye ligi hiyo ni pamoja na mshambulizi Sadio Mane anayechezea Al Nassr na Kalidou Koulibaly anayesakatia Al Hilal.

Senegal wataanza kutetea ubingwa wao wa AFCON kwa kucheza na majirani zao Gambia.