Nyumbani! Jadon Sancho aadhimisha kurejea kwake Borussia Dortmund kwa assist nzuri

Mashabiki wa Dortmund walimkaribisha tena kwa kelele, makofi na shangwe na kumfanya ajisikie yuko nyumbani tena.

Muhtasari

•Sancho alisaidia Dortmund kushinda 3-0 dhidi ya Darmstadt katika mechi yake ya kwanza pale  tangu ajiunge nao tena kutoka Man United siku chache zilizopita.

•Sancho aliingizwa uwanjani katika dakika ya 55 ya mechi akichukua nafasi ya mshambuliaji chipukizi Jamie Bynoe-Gittens

alitoa assist nzuri kwa Marco Reus
Sancho alitoa assist nzuri kwa Marco Reus
Image: INSTAGRAM// BORRUSIA DORTMUND

Winga Jadon Sancho alithibitisha upendo wake kwa Borrusia Dortmund baada ya kuisaidia klabu hiyo ya Bundesliga kushinda 3-0 dhidi ya Darmstadt katika mechi yake ya kwanza pale  tangu ajiunge nao tena kutoka Manchester United siku chache zilizopita.

Dortmund ilithibitisha kuwasili kwa Sancho mnamo Alhamisi, Januari 11, baada ya winga huyo mwenye umri wa miaka 24 kukubali kujiunga nao kwa mkopo hadi mwisho wa msimu wa 2023/24.

Ili kuadhimisha kurejea kwake, mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alitoa pasi ya bao kwa kiungo Marco Reus kufunga bao la pili kwa Borrusia Dortmund siku ya Jumamosi jioni. Alikuwa amecheza kwa takriban dakika 22 tu kabla ya kutoa pasi nzuri ya bao.

Sancho aliingizwa uwanjani katika dakika ya 55 ya mechi akichukua nafasi ya mshambuliaji chipukizi Jamie Bynoe-Gittens. Mashabiki wa Borussia Dortmund walimkaribisha tena kwa kelele, makofi na shangwe na kumfanya ajisikie yuko nyumbani tena.

Sancho alijiunga tena na Borrusia Dortmund siku ya Alhamisi baada ya kupoteza nafasi yake ya kucheza Manchester United. Alijiunga na Mashetani Wekundu mwezi Julai 2021  ila akapoteza nafasi yake mwaka jana baada ya kutofautiana na kocha Erik ten Hag.

Siku ya Alhamisi, United ilithibitisha kwamba staa huyo wa soka mwenye umri wa miaka 23 amejiunga tena na klabu yake ya zamani. Mkataba uliokubaliwa na klabu hizo mbili una thamani ya pauni milioni 3.4 na klabu ya Borrusia inatarajiwa kugharamia sehemu ya mshahara wa mshambuliaji huyo.

Uhamisho wa Sancho hata hivyo sio wa kudumu kwani amejiunga tena na timu hiyo ya Ujerumani kwa mkopo hadi mwisho wa msimu wa EPL 2023/24.

"Sancho sasa atarejea Ujerumani kwa muda huku Borussia Dortmund wakijiandaa kuanza tena kampeni yao ya Bundesliga baada ya mapumziko ya msimu wa baridi. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza aliyecheza mechi za kimataifa 23 anaondoka na tunawatakia heri katika kipindi kilichosalia cha msimu huu,” Man United ilisema katika taarifa iliyotumwa kwenye tovuti yake rasmi.

Borrusia Dortmund pia ilithibitisha kurejea kwa winga huyo mwenye umri wa miaka 24 na kufichua kwamba atasalia katika klabu hiyo hadi Juni 30, 2024.

Wakati akitangaza kurejea kwake, mchezaji huyo alisema anajivunia sana kujiunga tena na klabu hiyo ya Ujerumani na kusema kwamba ana hamu ya kuicheza tena.

“Halo mashabiki wa BVB. Hapa ni kwa Jadon. Nataka tu kusema heri ya mwaka mpya. Nimefurahi sana kurejea na siwezi kusubiri kuanza. Ona uone na utunze,” Sancho alisema kwenye video aliyorekodi.

Inaripotiwa kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alitaka sana kuondoka United na hata inasemekana ndiye aliyesukuma kabisa uhamisho huo wa kwenda kujiunga na Borussia Dortmund.

Hii ni baada ya kutofautiana na kocha wa Manchester United, Erik Ten Hag, na kupelekea kutengwa kutoka kwenye kikosi hicho.