Wanahabari wa Ghana na Misri wakabiliana kwa maneno wakati wa mechi ya AFCON (Video)

"Sisi si majasusi. Sisi ni waandishi wa habari walioidhinishwa. Ujumbe wa Misri ulituita majasusi nje ya lango, na polisi walituzuia hadi walipoingilia kati kwa niaba yetu." mwanahabari wa Ghana aliteta.

Muhtasari

• Mechi hiyo kati ya Misri na Ghana iliishia kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Raia wa Ghana
Raia wa Ghana
Image: FACEBOOK//CAF

Kabla ya kipute cha AFCON baina ya Black Stars ya Ghana na The Pharaohs ya Misri, kizaazaa kilishuhudiwa baina ya wanahabari wa spoti kutoka pande zote mbili.

Kwa kawaida, kila taifa linaloshiriki katika mashindano hayo ya AFCON nchini Ivory Coast limepeleka wanahabari wao wa spoti kufuatilia kinyang’anyiro hicho na haswa kutoa kila ripoti kuhusu timu yao ya nyumbani.

Wakati timu za mataifa hayo mawili zinajiandaa, wanahabari walikabiliana kwa maneno nusra kushikana mashati kabla ya kutawanywa.

Wanahabari wa Ghana waliwatuhumu wenzao wa Misri kwa kuwanyanyapaa na kuwataja kama wapelelezi ambao walitumwa kudokoa taarifa muhimu kutoka kwa kambi ya Misri.

Hata hivyo, wanahabari wa Ghana walizuiliwa mpaka pale maafisa wa shirikisho la soka barani Afrika CAF lilipoingilia kati na kuwaruhusu kuingia uwanjani.

Mwanahabari mmoja wa Ghana alisikika akiteta vikali kwamba wenzao wa Misri waliwaita wapelelezi licha ya kuwa wao ni wanahabari walioidhinishwa na kuwataka watengue kauli hiyo mara moja kwani nchini kwao [ Ghana] ntu kuitwa mpelelezi ni kinyume cha sheria.

"Sisi si majasusi. Sisi ni waandishi wa habari walioidhinishwa. Ujumbe wa Misri ulituita majasusi nje ya lango, na polisi walituzuia hadi walipoingilia kati kwa niaba yetu. Tafadhali waambie sisi si wapelelezi." Alisema.

Baadhi ya mashabiki katika video hiyo ambayo imevutia maoni mseto wanahisi kwamba raia wa mataifa ya ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, haswa mataifa ya waarabu wana hulka ya kuwanyanyapaa wenzao weusi.

Wengine walitaka wanahabari wa Misri pia kupigwa marufuku kutotia maguu yao nchini Ghana hadi pale watakapotengua kauli yao ya kuwataja wenzao kama majasusi.

“Ikiwa GFA imeona video hii wanapaswa kulipiza kisasi na wasiruhusu Wanahabari wowote wa Misri kwenye uwanja wetu wa mafunzo rahisi.” Mmoja alisema.

“Hiyo ingesikika kama tunabishana. Watu hao ni wabaguzi wa rangi, lakini hatuwapi hata kidogo. Ningeshauri tulipize kisasi kesho uwanjani.” Mwingine alisema.