AFCON 2023: Tanzania yapokwa ‘tonge mdomoni’ na Zambia

Zambia ilipata pigo kwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa nahodha wao Rodrick Kabwe katika dakika ya 44.

Muhtasari

•Bao la dakika ya 88 la Zambia limefuta matumaini ya Tanzania kuandikisha ushindi wa kwanza katika michuano ya Afcon.

•Hii ni sare ya pili kwa Tanzania katika michuano ya AFCON.

Image: BBC

Bao la dakika ya 88 la Zambia limefuta matumaini ya Tanzania kuandikisha ushindi wa kwanza katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (Afcon).

Tanzania iliandikisha goli la kwanza katika dakika ya 11 kupitia winga wake wa kimataifa Simon Msuva akiunganisha pasi maridhawa kutoka kwa nahodha Mbwana Samatta.

Zambia ilipata pigo kwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa nahodha wao Rodrick Kabwe katika dakika ya 44.

Tanzania iliendelea kuutawala mchezo huo na kukosa nafasi kadhaa za wazi kuongeza goli la pili wakati Zambia ikicheza mchezo wa kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Mashambulizi hayo ya kushtukiza yalizaa matunda katika dakika ya 88 ambapo mshambuliaji wa klabu ya Leicester City ya England Patson Daka alipofunga bao la kusawazisha kwa kichwa kikali akiunganisha krosi ya Clatous Chota Chama anayechezea klabu ya Simba ya Tanzania.

Hii ni sare ya pili kwa Tanzania katika michuano ya AFCON. Sare ya kwanza waliipata kwa Ivory Coast katika michuano ya mwaka 1980 ambapo magoli yalikuwa 1-1. Katika michuano ya mwaka 2019 Tanzania ilipoteza michezo yote mitatu.

Kwa matokeo hayo sasa Tanzania inaendelea kushikilia mkia wa kundi Fwakiwa na alama moja huku Zambia na DRC wakiwa na alama mbili kila mmoja na kinara wa kundi ni Morocco wenye alama nne. Morocco na DRC walitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa awali wa kundi hilo.

Tanzania sasa itaminyana na DRC siku ya Jumatano katika mchezo wa mwisho wa makundi, Morocco na Zambia pia wataminyana siku hiyo. Mpaka sasa hakuna timu yoyote katika kundi hilo ambayo imekata tiketi ya kucheza katika hatua ifuatayo