AFCON 2023: Tazama matokeo ya Jumatatu, ratiba ya michuano ya Jumanne

Mechi za mwisho za Kundi A na B zilishuhudia Guinea Bissau na Msumbiji zikitolewa rasmi kwenye michuano hiyo.

Muhtasari

•AFCON 2023 iliingia raundi ya tatu siku ya Jumatatu, Januari 22, huku mechi nne zikichezwa katika viwanja viwili tofauti nchini Ivory Coast.

• Nigeria iliua matumaini ya Guinea Bissau kufuzu kwa raundi ifuatayo baada ya kuwalaza 1-0. 

walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi A
Ivory Coast walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi A
Image: AFCON

Michuano inayoendelea ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) iliingia raundi ya tatu siku ya Jumatatu, Januari 22, huku mechi nne zikichezwa katika viwanja viwili tofauti nchini Ivory Coast.

Mechi za mwisho za Kundi A na Kundi B zilishuhudia Guinea Bissau na Msumbiji zikitolewa rasmi kwenye michuano hiyo huku Ivory Coast na Ghana waliomaliza katika nafasi ya tatu katika Kundi A na Kundi B mtawalia sasa zikingoja matokeo kutoka kwa makundi mengine ili kujua iwapo zitafuzu kwa hatua inayofuata.

Wenyeji, Ivory Coast walilazimika kushika nafasi ya tatu ya kundi A baada ya kupata kipigo kikubwa cha mabao 4-0 dhidi ya Equatorial Guinea katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Stade Olympique Alassane Quattara saa mbili usik. Mshambulizi Emilio Nsue (2), kiungo wa kati Pablo Ganet na Jannick Buyla walifunga mabao manne kwa Equatorial Guinea huku Ivory Coast ikifunga mabao mawili yaliyokataliwa kwa kuotea.

Wakati huo huo, Nigeria iliua matumaini ya Guinea Bissau kufuzu kwa raundi ifuatayo baada ya kuwalaza 1-0. Bao pekee katika mechi hiyo lilikuwa la kujifunga la beki Opa Sangate.

Cape Verde na Misri zimefuzu kwa raundi inayofuata ya AFCON 2023 licha ya kutoka sare ya 2-2 katika uwanja wa Stade Felix Houphouet-Boigny mjini Abijan. Benchimol na Bryan Teixeira waliifungia Cape Verde huku Trezeguet na Mostafa Mohamed wakiifungia Misri.

Msumbiji kwa upande mwingine walitoka katika michuano hiyo licha ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Ghana kwenye uwanja wa Stade Olympique Alassane Quattara. Jordan Ayew aliifungia Ghana mabao mawili kabla ya Geny Catamo na Reinildo Mandava kuifungia Msumbiji mabao mawili kuelekea mwisho wa mchezo.

Mechi zingine nne zitachezwa Jumanne saa mbili usiku na saa tano jioni.

Tazama ratiba ya mechi za Jumanne;

Gambia vs Cameroon  (Saa mbili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade de la Paix (Bouake))

Guinea vs Senegal (Saa mbili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Charles Konan Banny (Yamoussoukro))

Angola vs Burkina Faso (Saa tano usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Charles Konan Banny (Yamoussoukro))

Mauritania vs Algeria (Saa tano usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade de la Paix (Bouake))