Man United kumkosa Anthony Martial kwa kipindi kirefu kufuatia upasuaji mkubwa

Kulingana na kipindi chake cha kupona na mkataba wake ukiisha hivi karibuni, huenda akawa ameichezea United mechi yake ya mwisho.

Muhtasari

‚ÄĘKulingana na Mashetani Wekundu, mwanasoka huyo alifanyiwa upasuaji huo mkubwa ili kurekebisha tatizo la kinena.

Mshambulizi Anthony Martial
Mshambulizi Anthony Martial
Image: GETTY IMAGES

MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Anthony Martial amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kinena chake.

Habari za kufanyiwa upasuaji wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 zilitolewa na klabu hiyo ya EPL mnamo Jumatano alasiri kupitia tovuti yake rasmi.

Kulingana na Mashetani Wekundu, mwanasoka huyo wa kimataifa wa Ufaransa alifanyiwa upasuaji huo mkubwa ili kurekebisha tatizo la kinena. Sasa atakuwa nje kwa zaidi ya miezi miwili.

"Mshambulizi wa Manchester United Anthony Martial amekamilisha upasuaji uliofaulu kushughulikia matatizo yake ya kinena na atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki 10 atakaporejea," ilisema taarifa ya Man United.

Waliongeza, "Tunamtakia Anthony apone haraka na tunatazamia kurejea kwake."

Wiki iliyopita, vyombo vya habari vya Uingereza vilifichua kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aliambiwa afanye mazoezi peke yake ili kuboresha hali yake kabla ya kuchaguliwa tena na meneja Erik ten Hag.

Martial hata hivyo amekuwa akilalamika kuhusu suala la paja, ambalo United wamethibitisha kuwa amefanyiwa upasuaji katika jitihada za kutatua suala hilo. Huenda asipatikane hadi mwanzoni mwa Aprili.                                                

Hata hivyo, huku mkataba wake ukielekea kumalizika mwishoni mwa msimu huu, na tayari Mfaransa huyo akiwa tayari ameanza kutengwa kwenye kikosi hicho, kuna uwezekano mkubwa kwamba ameichezea klabu hiyo mechi yake ya mwisho.