logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Afcon 2023: Wachezaji 6 wanaoweza kunyakuliwa na klabu kubwa Ulaya baada ya mashindano

Wanne kati yao bado hawajacheza katika ligi yoyote kati ya ligi tano bora za Ulaya. Na watatu wakiwa wenye umri wa miaka 22 au chini ya hapo.

image
na Samuel Maina

Michezo01 February 2024 - 11:51

Muhtasari


  • •Wanne kati yao bado hawajacheza katika ligi yoyote kati ya ligi tano bora za Ulaya. Na watatu wakiwa wenye umri wa miaka 22 au chini ya hapo.

Vilabu barani Ulaya vinafuatilia wachezaji waliofanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, ambapo timu za chini zimeonyesha kiwango kizuri.

Wakati kombe hilo likielekea katika hatua ya robo fainali, BBC Sport Africa imechagua nyota sita ambao huenda wakanyakuliwa na vilabu vikubwa vya Ulaya.

Wanne kati yao bado hawajacheza katika ligi yoyote kati ya ligi tano bora za Ulaya. Na watatu wakiwa wenye umri wa miaka 22 au chini ya hapo.

Dirisha la uhamisho la wachezaji linakaribia kufungwa siku ya Alhamisi, huenda muda si mrefu wanunuzi wataanza kuwasilisha zabuni zao.

Lamine Camara, Senegal

Lamine Camara kutoka klabu ya Metz ya Ufaransa na taifa la Senegal, ni kiungo wa kat. Ametajwa kuwa Mwanasoka Bora Chipukizi wa Bara la Afrika mwezi Disemba, Camara mwenye umri wa miaka 20 alijitangaza kwa kufunga mabao mawili na kuwa mchezaji bora wa mechi katika ushindi wa Senegal wa 3-0 dhidi ya Gambia.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Camara kufunga mabao mawili katika mchezo mmoja kwenye mashindano ya kimataifa.

Alifunga mabao mawili wakati Senegal ya Afrika Magharibi ilipoishinda Tunisia katika Afcon ya vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2023, huku pia akiwa katika kikosi ya wakubwa kilichotwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika mwaka jana.

Kiungo wa kati ambaye ni zao la akademi ya Senegal ya Generation Foot, ambayo imezalisha wengine kama Sadio Mane - alifanikiwa kwa asilimia 84 ya pasi zake kabla ya Simba ya Teranga kutupwa nje ya michuano hiyo na Ivory Coast katika hatua ya 16 bora.

Camara alijiunga na Metz, Februari mwaka jana na kujitengenezea jina Oktoba kwa kufunga bao dhidi ya Monaco kwenye mechi ya Ligue 1.

Jesus Owono, Equatorial Guinea

Owono ni kipa wa Alaves ya Unispania na Equatorial Guinea, alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika sare ya kwanza ya Equatorial Guinea dhidi ya Nigeria na katika mechi ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Ivory Coast.

Owono alicheza bila kufungwa katika mechi tatu katika mechi nne za kombe la mataifa ya Afrika 2021 na kuokoa penalti mbili katika ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Mali na timu yake ikatinga robo-fainali.

Owono anaweza kuwa mlinda mlango mkubwa barani Afrika - akifuata nyayo za magwiji kama Carlos Kameni wa Cameroon na Thomas N'Kono na Vincent Enyeama wa Nigeria.

Emmam Ashour, Misri

Ashour ni mchezaji wa Al Ahly na Misri, alikuwa bora katika kutoa usaidizi wa ulinzi na kusonga mbele ili kuongeza mashambulizi ya Misri wakati wa mechi zao za Kundi B.

Licha ya kucheza kwa dakika chache zaidi ya wachezaji wenzake wengi, Ashour bado alimaliza akiwa kileleni kwa kutengeneza nafasi, pasi, kutamba na mpira , kukabiliana na adui - akiwa chini ya mchezaji Mostafa Mohamed.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alicheza kwa muda mfupi na mabingwa mara tatu wa Denmark, Midtjylland mwaka 2023, akifunga kwenye mechi yake ya kwanza ya Europa League na Superliga na kisha kuhama kwenda Zamalek ya Misri kwa ada ya pauni milioni 2.6.

Alirejea katika ligi kuu ya nchi yake akiwa na Al Ahly Julai mwaka jana. Je, ataweza kurudi tena katika klabu yoyote ya Ulaya?

Aboubakary Koita, Mauritania

Koita anayecheza Sint-Truiden ya Belgium na taifa la Mauritania alizitimiza ndoto za taifa lake kusonga mbele.

Mchezaji mwenye kasi, kinda huyo mwenye umri wa miaka 25, winga mwenye jicho la kulenga lango - aliisaidia Simba wa Chinguetti kutinga hatua ya 16 bora, na kujihakikishia ushindi wa kwanza kabisa kwenye michuano hiyo ilipowalaza mabingwa wa Afcon 2019 Algeria 1-0.

Roketi ya Koita ya bao la masafa marefu katika mechi waliyofungwa 3-2 na Angola wakati wa hatua ya makundi, litakuwa miongoni mwa mabao bora ya michuano hiyo.

Mzaliwa wa Senegal, Koita ni mchezaji wa Sint-Truiden ya Ubelgiji - nchi ambayo aliishi maisha yake ya ujana, baadaye alitumia miaka miwili akichezea mabingwa wa zamani Gent.

Gelson Dala, Angola

Dala ni mchezaji wa klabu ya Al Wakrah ya Qatar. Ameshinda mara nne na kuisaidia Angola kufuzu robo fainali kwa mara ya kwanza tangu 2010, na hivyo kumfanya kuwa nyuma kwa bao moja nyuma ya kinara Emilio Nsue.

Baada ya mabao mawili dhidi ya Mauritania katika hatua ya makundi, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alifunga mabao mengine mawili na kuweka bao katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Namibia katika hatua ya 16 bora.

Ufungaji wa Dala akiwa Angola akiwa kijana ulisababisha miamba ya Ureno, Sporting CP kumsajili mwaka 2017, lakini hakuweza kuingia kwenye kikosi chao cha kwanza na alikaa kwa msimu mmoja huko Rio Ave mnamo 2020-21.

Tangu ajiunge na klabu ya Al Wakrah ya Qatar mwaka 2022 amekuwa na wastani wa kufinga wa zaidi ya goli katika kila mchezo.

Aguibou Camara, Guinea

Umaliziaji wa Camara uliipa Guinea ushindi muhimu dhidi ya Gambia, na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amefanya kazi kubwa katika kila dakika ya mbio zao za robo fainali.

Mchezaji wa Atromitos ya Ugiriki, amepata uzoefu wa katika Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Ulaya tangu ajiunge na Olympiacos mwaka 2021 na kwa sasa yuko kwa mkopo katika timu ya Atromitos ya Ligi Kuu ya Ugiriki.

Mshambulizi huyo mahiri, ambaye pia anaweza kucheza katika safu ya kiungo, tayari ameshawekwa katika nafasi mbalimbali na Guinea wakati wa mechi zao, na alizungumzia utayari wake wa kubadili namba baada ya kuombwa na meneja Kaba Diawara wakati wa mechi za makundi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved