Inasikitisha! Dili ya mamilioni ya Omala na klabu ya Algeria yagonga ukuta dakika za mwisho

K’Ogalo ingeweka mfukoni zaidi ya Ksh3.2 milioni huku Omala akitarajiwa kupokea mshahara wa 1.3 milioni kila mwezi.

Muhtasari

•Gor walikuw wametangaza kwamba Omala angejiunga na JS Sauora kwa mkopo wa miezi sita lakini dili hiyo iligonga mwamba katika dakika za mwisho siku ya Jumatatu.

•Ripoti zinaashiria kutopatikana kwa nafasi za kigeni katika klabu hiyo ya Algeria kulisababisha uhamisho huo kutofua dafu.

Mshambulizi wa Gor Mahia Benson Omala
Image: HISANI

Mshambulizi mahiri wa Gor Mahia Benson Omala atasalia katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya na hatajiunga na klabu ya JS Sauora ya Algeria kama ilivyotarajiwa.

Gor Mahia walikuwa wametangaza hapo awali kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 22 angejiunga na JS Sauora kwa mkopo wa miezi sita lakini dili hiyo inaripotiwa kugonga mwamba katika dakika za mwisho siku ya Jumatatu.

Bado haijabainika kwa nini dili hiyo nzuri ilisambaratika lakini ripoti zinaonyesha kuwa kutopatikana kwa nafasi za kigeni katika klabu hiyo ya Afrika Kaskazini kulisababisha uhamisho huo kutofua dafu. Aidha, inaripotiwa kuwa JS Sauora walielekeza macho yao kwa mshambuliaji mwingine wa Cameroon, baada ya kibali cha Gor Mahia kuchelewa kufika.

Hiyo ina maana kwamba mshambuliaji huyo aliyejizolea sifa kemkem atasalia Gor Mahia hadi mwisho wa msimu wa 2023/24 wakati uhamisho mwingine utakapopendekezwa tena.

Siku ya Jumatatu, viongozi hao wa ligi ya Kenya walikuwa wametangaza kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22 angeihama klabu hiyo kwa mkopo.

“TANGAZO: Mshambulizi wetu Benson Omolla anahamia Saoura FC ya Algeria kwa mkataba wa mkopo. Kila la heri Omalla,” Gor Mahia ilitangaza kupitia mitandao ya kijamii.

Iwapo dili hiyo ingekamilika, K’Ogalo ingeweka mfukoni zaidi ya Ksh3.2 milioni kutoka kwa mkataba huo wa mkopo huku Omala akitarajiwa kupokea mshahara wa jumla wa $8,000 (Ksh 1.3 milioni) kila mwezi mara tu mkataba huo ukitiwa saini.