logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Jesse Lingard hatimaye apata klabu baada ya kupigwa na baridi kwa zaidi ya miezi 7

Lingard amekuwa bila klabu kwa zaidi ya miezi 7 tangu kandarasi yake na klabu ya Nottingham Forest ilipomalizika mwishoni mwa msimu wa 2022/23.

image
na Radio Jambo

Habari08 February 2024 - 09:38

Muhtasari


•Lingard amekuwa bila klabu kwa zaidi ya miezi 7 tangu kandarasi yake na klabu ya Nottingham Forest ilipomalizika mwishoni mwa msimu wa 2022/23.

•Alisema dhamira ya FC Seoul ya kutaka kumsajili kabla ya uhamisho huo kujulikana kwa umma siku ya makataa nchini Uingereza ilisaidia kumshawishi kuhama.

amejiunga na FC Seoul

Kiungo wa kati wa zamani wa Manchester United Jesse Lingard amekamilisha uhamisho wa kujiunga na klabu ya FC Seoul ya Korea Kusini.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 31 amekuwa bila klabu, akifanya mazoezi ya kibinafsi kwa zaidi ya miezi saba tangu kandarasi yake na klabu ya Nottingham Forest ilipomalizika mwishoni mwa msimu wa 2022/23.

Ripoti kutoka Ulaya zinasema kuwa kiungo huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ya Korea Kusini, huku kukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Wakati akizungumzia uhamisho huo, Lingard alisema alipokea ofa nyingi lakini hatimaye akaamua kuwa anataka uzoefu mpya wa soka nchini Korea Kusini.

"Siku zote nilitaka changamoto tofauti na kuunda kumbukumbu mpya katika kazi yangu," Lingard alisema kwenye video.

Aliongeza, "Ninaamini Korea Kusini ni mahali pazuri kwa hilo."

Mchezaji huyo alisema dhamira ya FC Seoul ya kutaka kumsajili kabla ya uhamisho huo kujulikana kwa umma siku ya makataa nchini Uingereza ilisaidia kumshawishi kuhama.

"FC Seoul walinionyesha upendo mkubwa, wakinitumia ofa halisi kwenye karatasi huku vilabu vingine vilipokuwa vikiwasiliana nami kwa maneno. Pia walikuja Manchester kuangalia hali yangu ya kimwili pia," alisema.

Wakati wa siku zake kuu, Lingard aliichezea Manchester United kuanzia 2014 hadi 2022 wakati alipojiunga na Nottingham Forest baada ya mkataba wake na klabu yake ya utotoni kuisha. Kwa miaka minane aliyoichezea Man United, alishirikishwa kwenye 232 akifunga mabao 35 huku akiisaidia United kushinda Kombe la FA, Kombe la Ligi na Ligi ya Europa.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 baadaye alijiunga na Forest kwa mkataba wa mwaka mmoja Julai 2022 baada ya mkataba wake kumalizika. Nottingham Forest ilimwachilia Juni mwaka jana baada ya kucheza mechi 20.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved