Afcon: Fahamu mamilioni , zawadi za thamani wachezaji wa Ivory Coast na Nigeria walipewa na serikali zao

Wachezaji wa Nigeria pia hawakuachwa hivyo na serikali yao kwani watapokea zawadi ya pesa na vitu vingine vya thamani.

Muhtasari

•Rais wa Ivory Coast Allassane Outtarra alitangaza kuwa watapata pia na nyumba za kifahari zenye thamani ya kiasi sawa cha pesa watakazopokea.

•Wachezaji wa Super Eagles pia walipewa heshima ya kifahari ya Mwanachama wa Order of the Niger (MON).

Fahamu mamilioni , zawadi za kifahari wachezaji wa Ivory Coast na Nigeria walipewa na serikali zao
Afcon 2023: Fahamu mamilioni , zawadi za kifahari wachezaji wa Ivory Coast na Nigeria walipewa na serikali zao
Image: HISANI

Kila mmoja wa wachezaji 27 katika timu ya Ivory Coast  iliyoshinda AFCON 2023 atapata zawadi ya pesa ya $82,000 (Ksh 12.6m) kutoka kwa serikali ya taifa hilo la Afrika Magharibi.

Wakati akiwasherehekea wachezaji hao siku ya Jumanne kwa kushinda kombe hilo la kifahari la kandanda la Afrika mnamo Jumapili usiku, rais wa Ivory Coast Allassane Outtarra alitangaza kuwa watapata pia na nyumba za kifahari zenye thamani ya kiasi sawa cha pesa watakazopokea.

"Mmeleta furaha kwa Wana-Ivory  Coast wote,  hongera, hongera," alisema Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya Afrika nzima.

Kocha wa muda wa timu ya taifa ya kandanda ya Ivory Coast, Emerse Fae, ambaye alichukua usukani  katika hatua ya 16 bora kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha Jean-Louis Gasset, upande wake alitunukiwa dola 164,000 (Ksh27.2milioni).

Wachezaji wa Nigeria pia hawakuachwa hivyo na serikali yao kwani watapokea zawadi ya pesa na vitu vingine vya thamani ikiwa ni pamoja na viwanja na nyumba katika moja ya miji mikubwa nchini humo, Abuja.

Wachezaji wa Super Eagles ambao walichapwa 2-1 na Ivory Coast Jumapili jioni na kupata tuzo ya fedha pia walipewa heshima ya kifahari ya Mwanachama wa Order of the Niger (MON).

Kufuatia mwisho wa mashindano ya AFCON 2023, mshindi Ivory Coast alituzwa $7m (Ksh1.1 bilioni), washindi wa pili walipata Nigeria $4m (Ksh 636m) huku, Afrika Kusini na DR Congo waliofuzu nusu fainali kila moja wakipata $2.5m ( 397.5m), huku timu nne zilizofuzu robo fainali zikitwaa $1.3m (Ksh206.7m) kila moja.