Kwa mara nyingine tena, klabu ya Chelsea imeelekeza uvamizi wake katika kambi ya klabu cha Brighton na kuwapora chuma chao, katika msururu ambao umekuwa ukiendelea tangu uongozi mpya wa Chelsea kuchukua usukani.
Taarifa za hivi punde ni kwamba Chelsea wamemkwapua mkuu wa usajili wa Brighton, Sam Jewell – akiwa ni mtu wa 11 kuondoka Brighton na kujiunga na Chelsea katika kipindi cha miezi 17 iliyopita.
Jewell atakuwa sehemu ya mradi wa vilabu vingi chini ya uongozi wa BlueCo kuleta na kuchagua wachezaji wapya wa Chelsea na vilabu Zaidi.
Itakumbukwa kwamba tangu Chelsea wapate uongozi mpya chini ya Todd Boehly, Behdad Eghbali na José E. Feliciano ambao walishikana kikoa kuinunua The Blues kutoka kwa Mrusi Roman Abrahamovic, klabu hiyo imekuwa ikiipora Brighton watu mbalimbali kutoka kwa wachezaji, kocha na hata wafanyikazi wengine.
Baada ya kumfuta Thomas Tuchel, Chelsea walimwendea kocha Graham Potter mwaka 2022 na kumfuta kazi miezi michache baadae kufuatia msururu wa matokeo mabaya.
Kando na kocha Potter, Chelsea pia wameipora Brighton wachezaji Marc Cucurella ambaye ni beki, mlinda lango Robert Sanchez na kiungo ghali Zaidi Moises Caicedo.
Lakini pia walichukua baadhi ya wafanyikazi wao katika klabu wakiwemo Paul Winstanley, Billy Reid, Björn Hamberg, Bruno Saltor, Ben Roberts, Kyle McCauley na sasa, Sam Jewell.