Arsenal yaandikisha rekodi kubwa kwenye EPL baada ya kuipiga Sheffield United 0-6

Wanabunduki kwa sasa wamekalia nafasi ya tatu ya jedwali la EPL 2023/24 wakiwa wamejizolea pointi 61.

Muhtasari

•Waliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya EPL kushinda kwa mabao matano au zaidi katika mechi tatu mfululizo za ugenini.

•Liverpool wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 63 huku vinara Manchester City wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 62.

Image: TWITTER// ARSENAL

Arsenal FC iliandikisha rekodi kubwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuiadhibu Sheffield United 0-6 kwenye uwanja wa Bramall Lane siku ya Jumatatu usiku.

Wanabunduki waliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu kushinda kwa mabao matano au zaidi katika mechi tatu mfululizo za ugenini.

Awali walikuwa wameshinda 0-5 na 0-6 ugenini dhidi ya Burnley na West Ham United mtawalia.

Nahodha Martin Odegaard alitangulia kuifungia klabu hiyo yenye maskani yake jijini London Jumatatu usiku katika dakika ya 5 kabla ya mabao mengine matatu kufungwa katika kipindi cha kwanza. Bao la kujifunga la beki Jayden Bogle katika dakika ya 13 lilifanya matokeo kuwa 0-2 kabla ya washambuliaji Gabriel Martinelli na Kai Havertz kuongeza Arsenal bao moja kila mmoja.

Bao moja pekee lilifungwa katika kipindi cha pili huku kiungo Declan Rice akimalizia pasi maridadi kutoka kwa mshambulizi Bukayo Saka. Hii ihata hivyo lihitimisha mbio za wanabunduki za kufunga mabao 2+ katika vipindi saba mfululizo vya EPL.

Wanabunduki kwa sasa wako katika nafasi ya tatu ya jedwali la EPL 2023/24 wakiwa wamejizolea pointi 61 katika mechi 27 zilizochezwa tayari.

Liverpool wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 63 huku washindi wa EPL 2022/23, Manchester City wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 62.

Ni michezo 11 pekee iliyosalia hadi mwisho wa msimu wa 2023/24 na kinyang'anyiro cha kuwania taji kinaonekana kuwa kigumu sana na cha kuvutia huku wababe hao watatu wakipambana kuona nani ataenda nyumbani na kombe mwishoni mwa msimu huu.