Kevin De Bruyne akanusha madai kwamba Jose Mourinho ndiye alimfukuza Chelsea

Kwa muda mrefu, mashabiki wa Chelsea wamekuwa wakihisi kwamba Mourinho ndiye aliyewauza De Bruyne na Mohamed Salah,

Muhtasari

• Kijana huyo Mbelgiji alisema kwamba pengine ni yeye alikosa subira katika kikosi cha Chelsea lakini kocha Mourinho alikuwa anamtaka sana kusalia Stamford Bridge.

De Bruyne na Mourinho
De Bruyne na Mourinho
Image: Maktaba

Kwa mara ya kwanza, mchezaji nguli wa kiungo cha kati katika timu ya Manchester City, Kevin De Bruyne amefunguka upande wake kuhusu kuondoka kwake Chelsea kipindi cha ukufunzi wake Mreno Jose Mourinho.

Akizungumza na Rio Ferdinand kwenye podkasti ya FIVE, De Bruyne amekanusha madai ambaye kwa muda mrefu yamekuwa yakiendelezwa mitandaoni kwamba kocha Jose Mourinho ndiye aliyechangia kuondoka kwake Chelsea.

Kijana huyo Mbelgiji alisema kwamba pengine ni yeye alikosa subira katika kikosi cha Chelsea lakini kocha Mourinho alikuwa anamtaka sana kusalia Stamford Bridge.

"Nilisaini Chelsea nikijua kwamba ningetolewa kwa mkopo mwaka wa kwanza na ikiwa nitafanya vizuri, basi tungeona nini kitatokea," alisema.

"Nilikuwa na mwaka mzuri sana huko Bremen, kisha wakati wa kiangazi kulikuwa na mzozo kidogo. Ningeweza kwenda Dortmund na Klopp au kubaki Chelsea, Jose alitaka nibaki, haikufanikiwa, labda sikuwa na subira wakati huo pia lakini nilitaka kucheza mpira tu.”

Alikiri kuwa ni timu kubwa yenye nyota wa juu, na kama mchezaji mchanga, alielewa angeweza kwenda kwa mkopo mara nyingi, lakini hakutaka hilo, na alisukuma kuuzwa.

Kwa muda mrefu, mashabiki wa Chelsea wamekuwa wakihisi kwamba Mourinho ndiye aliyewauza De Bruyne na Mohamed Salah, ambao wote wanashamiri Manchester City na Liverpool, huku The Blues wakijutia kuondoka kwao.