Haaland na Alexander-Arnold watupiana vijembe kuelekea mtanange wa Liverpool Vs Mancity

"Nimekuwa hapa mwaka mmoja, na nikashinda mataji matatu, na ilikuwa ni hisia nzuri sana. Sidhani kama anajua vizuri hisia hizi," Haaland alimjibu Trent Alexander-Arnold.

Muhtasari

• Liverpool wameiacha Mancity nyuma kwa pointi moja kuelekea kipute kikali baina ya timu hizo mbili wikendi hii.

Haaland na Trent watupiana maneno
Haaland na Trent watupiana maneno
Image: Facebook

Mshambuliaji matata wa Manchester City na beki wa kulia wa Liverpool Alexander Arnold wametia uchachukuelekea mtanange mkubwa Zaidi baina ya timu hizo mbili wikendi hii ugani Anfield.

Mechi ya Liverpool na Manchester City inatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwani huenda ndio itaanza kubainisha taji la ligi kuu msimu huu litaelekea wapi, Liverpool ikiwa imeiacha Mancity nyuma kwa pointi moja huku Arsenal ikiwa inazivizia timu hizo pia kwa point mbili nyuma ya Liverpool na moja nyuma ya Man City.

Trent Alexander-Arnold katika mahojiano na ESPN, alisema kwamba licha ya Mancity kushinda mataji mengi kuliko Liverpool katika kipindi cha kama miaka 7 iliyopita, wao [Liverpool] wako katika nafasi nzuri ya kufurahia mataji yao kuliko Mancity.

Trent alitaja utofauti mkubwa wa kifedha ambao umekuwa katika vilabu hivyo viwili akisema Mancity wametumia pesa nyingi katika kipindi hicho kupata mataji ilhali Liverpool walitumia hela kidogo kupata mataji, hivyo kwao mataji yao yana umuhimu kuliko kwa Man City.

"Tukikumbuka enzi hizi, ingawa [City] wameshinda mataji mengi kuliko sisi na pengine wamefanikiwa zaidi, mataji yetu yatakuwa na maana zaidi kwetu na kwa msingi wa mashabiki wetu kwa sababu ya hali ya kifedha ya vilabu vyote viwili," alisema ESPN.

Akimujibu, Haaland aijipiga kifua na kusema kwamba alikuja mwaka jana tu na tayari ameshinda mataji matatu kwa mpigo na Mancity ndani ya msimu mmoja, akisema kwamba anatilia shaka iwapo Arnold amewahi pata hisia kama hizo.

"Kama anataka kusema hivyo, sawa. Nimekuwa hapa mwaka mmoja, na nikashinda mataji matatu, na ilikuwa ni hisia nzuri sana. Sidhani kama anajua vizuri hisia hizi," Haaland aliiambia Sky Sports siku ya Alhamisi.

City walishindi Ligi Kuu, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa mwaka jana.