Unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi wafanya winga wa Brazil Vinicius Jr ahisi 'hataki kucheza'

Msimu uliopita kulikuwa na matukio 10 ya aina hiyo dhidi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23.

Muhtasari

•Vinicius Jr anasema anahisi "kana hatakii kucheza " kandanda kwa sababu ya unyanyasaji wa mara kwa mara wa kibaguzi aliofanyiwa.

•Vinicius alisema: "Haikuniingia akilini [kuondoka Uhispania] kwa sababu nikiondoka Uhispania nitawapa wabaguzi kile wanachotaka.

Vinicius Jr
Image: BBC

Winga wa Brazil Vinicius Jr anasema anahisi "kana kwamba hataki kucheza " kandanda kwa sababu ya unyanyasaji wa mara kwa mara wa kibaguzi aliofanyiwa.

Msimu uliopita kulikuwa na matukio 10 ya aina hiyo dhidi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 yaliyoripotiwa kwa waendesha mashtaka na La Liga.

Wakati wa mkutano wa wanahabari wenye hisia siku ya Jumatatu, Vinicius aliongeza kuwa hatalazimishwa kuondoka Real Madrid na Uhispania na kuruhusu ubaguzi wa rangi kushinda.

Hata hivyo, alisema alikuwa anaona ni "vigumu kusonga mbele" kutokana na unyanyasaji huo.

Brazil itamenyana na Uhispania katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid siku ya Jumanne kama sehemu ya kampeni ya kupinga ubaguzi wa rangi chini ya kauli mbiu 'Ngozi moja'.

Vinicius alisema: "Haikuniingia akilini [kuondoka Uhispania] kwa sababu nikiondoka Uhispania nitawapa wabaguzi kile wanachotaka.

“Nitabaki kwa sababu kwa njia hiyo wabaguzi wa rangi wanaweza kuendelea kuniona usoni zaidi na zaidi.

“Mimi ni mchezaji shupavu, nacheza Real Madrid na tunashinda mataji mengi na hilo haliwafurahishi watu wengi.

"Nataka tu kucheza kandanda lakini ni vigumu kusonga mbele; najihisi kutopenda kucheza."