Mourinho: Nilikuwa kocha Inter, Real, Chelsea na Porto, Katika vilabu vingine sikuwa kocha

Mourinho alisema kwamba vilabu hivyo 4 ndivyo alivyojihisi fahari kufunza lakini akapuuzilia vilabu vingine alivyowahi funza kama vile Manchester United, Tottenham Hotspurs na AS Roma.

Muhtasari

• "Nilikuwa kocha wa Inter, Real Madrid, Chelsea, Porto. Katika vilabu vingine, sikuwa kocha," alisema.

Jose Mourinho
Jose Mourinho
Image: AS ROMA

Mmoja kati ya wakufunzi wenye mafanikio makubwa Zaidi katika malimwengu ya soka ya karne ya 21, Jose Mourinho amefunguka baadhi ya vilabu ambavyo alihisi kuheshimika na kujisikia fahari kufunza.

Kwa mujibu wa nukuu kutoka kwa Mreno huyo ambazo zilichapishwa na mwanahabari wa michezo kutoka Italia, Fabrizio Romano, Mourinho alisema kwamba alijihisi fahari kuitwa kocha katika vilabu ambavyo aghalabu alishinda mataji ya kuheshimika.

Mourinho alivitaja vilabu kama Inter Milan ya Italia, Real Madrid ya Uhispania, Porto ya kwao Ureno na Chelsea ya Uingereza kama vilabu vilivyomheshimisha kama kocha.

Mreno huyo mwenye kauli tata hata hivyo alipuuzilia mbali vilabu vingine alivyofunza vikiwemo Manchester United ya Uingereza, Tottenham Hotspurs ya Uingereza na AS Roma ya Italia.

Alisema kwamba baada ya kufutwa kazi na Roma miezi michache iliyopita, bado atapata kazi lakini akataja kwamba atakuwa kocha na si vingine.

"Siku zote nitakuwa zaidi ya kocha".

"Katika vilabu vingine wewe ni kocha, katika vilabu vingine lazima uwe kocha, mkurugenzi wa ufundi, mkurugenzi wa mawasiliano, mtetezi wa klabu na wachezaji ... nataka kuwa kocha".

"Nilikuwa kocha wa Inter, Real Madrid, Chelsea, Porto. Katika vilabu vingine, sikuwa kocha," alisema.

Mourinho aliisaidia Porto kushinda taji la ligi ya mabingwa mwaka wa 2004, akaja Chelsea na kushinda mataji 3 ya ligi ya premia katika mikupuo miwili aliyohudumu, Real Madrid akashinda taji la La Liga na Inter Milan alishinda ligi ya mabingwa mwaka 2010.