Lionel Messi adai ameshatimiza kila ndoto ya utotoni katika taaluma yake yakandanda

Muargentina huyo ameshinda kila kitu kilichopo kwenye soka. Kombe la Dunia lilikosekana katika mkusanyiko wake wa kombe lakini hatimaye alishinda akiwa na Argentina mnamo 2022.

Muhtasari

• "Namshukuru Mungu alinipa mengi katika ngazi ya kitaaluma na kibinadamu, pamoja na familia yangu, marafiki zangu." Messi alisema.

Image: INSTAGRAM// LIONEL MESSI

Mchezaji anayetajwa kuwa nambari moja duniani kutokea Argentina, Lionel Messi ameweka wazi kwamba hana ndoto nyingine tena katika mali malimwengu ya soka kwani tayari anajiona kama ameshamaliza kila kitu.

Messi ambaye alikuwa anazungumza kwenye podikasti ya Big Time alisema kwamba kwa sasa anatarajia kustaafu kwani kila ndoto ya utotoni kwenye ulimwengu wa soka tayari ameshaitimiza, akijitaja kuwa miongoni mwa wachache wenye bahati ya kufanikisha hivyo.

"Katika kiwango cha michezo nilikuwa na bahati kuweza kufikia ndoto zangu zote na ukweli ni kwamba sikuweza kuuliza zaidi," Lionel Messi alisema kwenye podikasti ya Big Time alipoulizwa ikiwa ana ndoto zozote katika soka.

"Namshukuru Mungu alinipa mengi katika ngazi ya kitaaluma na kibinadamu, pamoja na familia yangu, marafiki zangu. Ninajaribu kufurahia kila kitu ambacho Mungu amenipa hadi sasa, ambacho ni kikubwa."

Muargentina huyo ameshinda kila kitu kilichopo kwenye soka. Kombe la Dunia lilikosekana katika mkusanyiko wake wa kombe lakini hatimaye alishinda akiwa na Argentina mnamo 2022.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alishinda mataji kumi ya La Liga, saba ya Vikombe vya Uhispania, saba vya Super Cup za Uhispania na mataji manne ya Ligi ya Mabingwa akiwa na Barcelona. Alishinda rekodi ya tuzo nane za Ballon d'Or.