Ndovu akaa kitako juu ya meza mara nyingine huku vita vya kuwania kombe la EPL vikichacha

Vijana wa Jurgen Klopp walikuwa na nafasi ya kusonga juu ya Arsenal Jumapili lakini walishindwa kuwapiga Man United

Muhtasari

•Wanabunduki walikwea juu ya meza tena Jumamosi jioni baada ya kuifunga Brighton 3-0 kwenye Uwanja wa Amex.

•Sare dhidi ya Manchester United iliwafanya Liverpool kufikisha pointi 71, sawa na Arsenal, lakini nyuma kwa mabao. 

Arsenal wanaongoza jedwali huku Liverpool na Man City wakifuata
Image: INSTAGRAM// PREMIER LEAGUE

Klabu ya soka ya Arsenal itasalia kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza kwa angalau siku sita zijazo baada ya Liverpool kukosa nafasi yake ya kupanda tena.

Wanabunduki, ambao katika siku za hivi majuzi wamepewa jina la utani ‘ndovu’ walikwea juu ya meza tena Jumamosi jioni baada ya kuifunga Brighton 3-0 kwenye Uwanja wa Amex. Ushindi huo uliwafanya kufikisha pointi 71, mbele ya Liverpool na Manchester City.

Mpinzani mwingine mkuu wa kombe la EPL 2023/24, Manchester City, alisalia katika nafasi ya tatu licha ya kushinda 4-2 dhidi ya Crystal Palace katika mechi iliyochezwa Selhurst Park Jumamosi alasiri. Ushindi huo uliwafanya kufikisha pointi 70, pointi moja tu nyuma ya Arsenal.

Vijana wa Jurgen Klopp walikuwa na nafasi ya kusonga juu ya Arsenal siku ya Jumapili lakini walishindwa kuwapiga Manchester United katika mechi ya kuburudisha sana iliyochezwa kwenye uwanja wa The Old Trafford. The Reds walitoka sare ya 2-2 dhidi ya Mashetani Wekundu, na kuchukua pointi moja tu huku vita vya kuwania taji la EPL 2023/24 vikizidi kuchacha.

Sare dhidi ya Manchester United iliwafanya Liverpool kufikisha pointi 71, sawa na Arsenal, lakini nyuma kwa mabao. Wanabunduki wana tofauti ya mabao 51 huku The Reds wakiwa na tofauti ya mabao 42.

Kwa hali ilivyo kwa sasa, Arsenal wanaongoza jedwali, wakifuatiwa na Liverpool, Man City wanashika nafasi ya tatu huku Tottenham Hotspurs wakishika nafasi ya nne. Kila timu ina mechi saba zaidi za kucheza kabla ya msimu kumalizika.

Mkiani mwa jedwali wamekalia Sheffield United wakiwa na pointi 16 pekee katika mechi 31 ilizocheza, Burnley wanashika nafasi ya 19 wakiwa na pointi 19 huku Luton Town wakishika nafasi ya 18 wakiwa na pointi 25.

Mechi zinazofuata za EPL zitachezwa wikendi ijayo.