Arsenal na Man City zafungasha virago katika Ligi ya Mabingwa Ulaya

Sasa hakuna timu ya kuwakilisha Uingereza katika nusu fainali ya mashindano hayo.

Muhtasari

•Mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa Ulaya Manchester City hatimaye wameondolewa katika kinyang’anyiro hicho mwaka huu.

•Arsenal pia iliondolewa baada ya kuchapwa na Bayern, hatua iliorudisha furaha na matumaini katika uwanja wa Allianz Arena.

Image: BBC

Mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa Ulaya Manchester City hatimaye wameondolewa katika kinyang’anyiro hicho mwaka huu baada ya kushindwa katika mechi ya robo fainali kupitia mikwaju ya penalti na mabingwa wa Uhispania Real Madrid katika uwanja wa nyumbani Etihad.

City ambao walijipata nyuma kwa bao moja lililofungwa mapema na Rodrygo , waliendelea kuvamia lango la wapinzani wao kabla ya kusawazisha dakika 14 kutoka mwisho wa muda wa kawaida wakati Kevin de Bruyne alipopata mpira kutoka kwa beki Antonio Rudiger aliyeshindwa kuuondoa katika eneo la hatari.

Ni matokeo ambayo Manchester City haikutarajia licha ya kutawala muda mrefu wa mechi hiyo , ambapo timu hiyo ya England ilikosa mshambuliaji wa moja kwa moja.

Wakati huohuo timu ya Arsenal pia iliondolewa katika michuano hiyo baada ya kuchapwa na Bayern Munich hatua iliorudisha furaha na matumaini katika uwanja wa Allianz Arena.

Bao kali la kichwa la Joshua Kimmich dakika ya 63 akiunganisha krosi ya Raphael Guerreiro lilitosha kuwavusha Wajerumani hao hadi nusu fainali kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya 2-2 mjini London katika mechi ya kwanza.

Licha ya kutoka sare kwenye Uwanja wa Emirates, Arsenal walikuwa na uhakika wa kusonga mbele dhidi ya Bayern Munich ambao walikuwa na msimu mbaya wa nyumbani na waliwakosa wachezaji muhimu kama vile Serge Gnabry na Kingsley Coman kwa sababu ya majeraha.