Xavi abadilisha msimamo, aamua kubaki kama kocha wa Barcelona msimu ujao

Meneja huyo alikuwa na mazungumzo yaliyofanikiwa na rais wa Barcelona, ​​Joan Laporta, na wajumbe wa bodi Jumatano.

Muhtasari

•Makamu wa rais wa Barcelona, Rafa Yuste alithibitisha uamuzi wa kubaki kwa kiungo huyo wa zamani na kueleza imani yao kwake.

•Xavi alikuwa ametangaza uamuzi wake wa kuondoka Barcelona mwishoni mwa msimu  baada ya kushindwa 5-3 na Villarreal mapema mwaka huu.

Kocha Xavi Hernandez
Image: HISANI

Meneja wa Barcelona Xavi Hernandez ataendelea kuinoa klabu hiyo ya Uhispania hata msimu ujao, licha ya awali kutangaza kwamba ataondoka mwishoni mwa msimu wa 2023/24.

Mabadiliko  ya msimamo ya meneja huyo mwenye umri wa miaka 44 yanakuja baada ya mazungumzo yaliyofanikiwa na rais wa Barcelona, ​​Joan Laporta, na wajumbe wa bodi siku ya Jumatano.

Makamu wa rais wa miamba hao wa Uhispania Rafa Yuste alithibitisha uamuzi wa kubaki kwa kiungo huyo wa zamani na kueleza imani yao kwake.

"Xavi atasalia, ana furaha na msisimko sana," Rafa Yuste, aliwaambia waandishi wa habari nje ya nyumba ya Laporta, ambapo majadiliano yalikuwa yamefanyika.

"Hatujawahi kufungua mazungumzo kwa kocha mwingine yeyote. Deco [Mkurugenzi wa Barça] anamwamini Xavi, amehakikishiwa,” aliongeza.

Hapo awali siku ya Jumatano, Xavi alikutana ana kwa ana na Deco, huku Laporta akishinikiza kumbakisha kocha mkuu baada ya majira ya kiangazi.

Klabu hiyo inatarajiwa kutoa tangazo rasmi hivi karibuni kuthibitisha kuwa nahodha wao wa zamani atasalia kuinoa timu hiyo msimu ujao, akiendelea na wadhifa huo ambao ameshikilia tangu Novemba 2021.

Hata hivyo bado haijabainika iwapo kandarasi yake itaongezwa kutoka tarehe yake ya mwisho ya Juni 2025. Rais wa klabu hiyo anatarajiwa kutoa taarifa zaidi katika mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi.

Xavi hapo awali alitangaza uamuzi wake wa kuondoka Barcelona mwishoni mwa msimu  baada ya kushindwa 5-3 na Villarreal mapema mwaka huu.

Licha ya kuwa na mkataba hadi mwisho wa msimu ujao, Xavi alitarajiwa kuondoka Camp Nou kabla ya mwisho wa Juni mwaka huu - lakini sasa amefanya mabadiliko makubwa.