Shirikisho la Soka nchini Kenya limeahirisha mechi mbili za ligi kuu ambazo zilipangwa kuchezwa Jumapili kutokana na mafuriko.
Nairobi City Stars ilipaswa kumenyana na Ulinzi Stars katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos huku Posta Rangers ikimenyana na Talanta FC katika uwanja huo huo.
"Mechi za Ligi Kuu ya FKF, Nairobi City Stars dhidi ya Ulinzi Stars na Posta Rangers dhidi ya Talanta FC zilizokuwa zichezwe leo katika Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos zimesitishwa kutokana na uwanja kujaa maji," shirika la utangazaji la taifa KBC ambalo lilipaswa kuangazia mechi moja kwa moja ilisema katika ilani.
"Tunaomba radhi kwa watazamaji wetu kwa usumbufu wowote uliojitokeza."
Nairobi City Stars vs Ulinzi Stars ilifaa kuanzia saa sita mchana huku mchujo kati ya Posta Rangers na Talanta FC ukichezwa saa tisa alasiri..
Katika mahojiano katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos, msimamizi wa mechi kati ya Ulinzi Stars dhidi ya Nairobi City Stars, Joseph Wajina, alisema tathmini ilionyesha kuwa uwanja haufai kuchezwa.
“Tulipokuja hapa asubuhi tulipima uwanja baada ya kikao chetu cha maandalizi ya mechi, tuliona uwanja hauchezeki. Takriban asilimia 80 ya uwanja umejaa maji,” Wajina alisema.
Alisema walifanya kikao kingine na wadau wote na kuhitimisha kuwa kusitishwa kwa mechi hizo ni jambo lisiloepukika.
Wajina alisema FKF itatoa njia ya kusonga mbele kufuatia kughairiwa kwa mechi hizo.
Afisa mkuu mtendaji wa Nairobi City Stars Patrick Korir alisema wanakaribisha uamuzi huo kwa ajili ya kuokoa wachezaji kutokana na majeraha.
Alisema uamuzi wa lini mechi hizo zitachezwa utafikiwa kwa kushauriana na wadau wote.
“Baada ya kikao chetu, tutafika kwenye shirikisho na Ligi na Mashindano zitaamua lini tutacheza. Kumbuka huu ulikuwa mchezo wa TV na hatuwezi kuamua sisi wenyewe. Tunaweza kuamua kucheza kesho lakini ninyi kama KBC hamko tayari,” akasema.
Kocha wa Nairobi City Stars Nicholas Muyoti alisema waliona uwanja huo kuwa hatari sana kwa wachezaji na ambao haungefanya mechi hizo kuwa za kufurahisha kwa watazamaji.
Muyoti hata hivyo alisema kughairiwa kunaweza kuathiri kisaikolojia kwa timu kwa kuwa walikuwa wamejiandaa vyema kwa mechi ya Jumapili.
"Morali ya wachezaji ilikuwa ya juu na tulitarajia matokeo mazuri katika mechi hii lakini hali ya hewa imefanya kushindwa kucheza hivyo tutajiandaa tena," alisema.
Mkufunzi wa Ulinzi Stars Anthony Kimani alikariri maoni yake akisema wachezaji wake walikuwa wakijiamini kabla ya mechi hiyo.
“Lakini sote tunaelewa kuwa mechi imeahirishwa kutokana na mazingira ambayo hayawezi kuepukika. Tunajua ukanda wa Afrika Mashariki umekuwa ukikumbwa na mvua kubwa ambayo imekwamisha shughuli nyingi,” alisema.