EPL yataja wachezaji 8 walioteuliwa kuwania tuzo la Mchezaji bora wa Msimu

Wateule nane wa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Msimu pia wametajwa.

Muhtasari

•EPL imealika kura kwa wachezaji 8 kutoka vilabu sita tofauti kabla ya kuamua ni nani atarejea nyumbani na tuzo hiyo mwishoni mwa msimu.

•Mashabiki wa soka wameombwa kumpigia kura mchezaji wao bora wa msimu wanayempenda kabla ya Jumatatu ya Mei 13, 2024.

Image: HISANI// PREMIER LEAGUE

Ligi kuu ya Uingereza imefichua wachezaji wanane watakaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu.

Ligi hiyo maarufu imealika kura kwa wachezaji wanane kutoka vilabu sita tofauti kabla ya kuamua ni nani atarejea nyumbani na tuzo hiyo mwishoni mwa msimu.

Wanane hao ni pamoja na nahodha wa Arsenal Martin Odegaard na kiungo Declan Rice, Phil Foden na Erling Haaland wa Manchester City, Cole Palmer wa Chelsea, Alexander Isak wa Newcastle, Olie Watkins wa Aston Villa na nahodha wa Liverpool Virgil van Dijk.

Mashabiki wa soka wameombwa kumpigia kura mchezaji wao bora wa msimu wanayempenda kabla ya Jumatatu ya Mei 13, 2024.

"Kura za umma zitaunganishwa na zile za jopo la wataalamu wa soka kuamua mshindi, ambaye atafichuliwa Jumamosi Mei 18," taarifa ya EPL ilisema.

Wateule nane wa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Msimu pia wametajwa.

Nane hao ni pamoja na Phil Foden na Erling Haaland wa Manchester City, Alexander Isak wa Newcastle, Cole Palmer wa Chelsea, Bukayo Saka na William Saliba wa Arsenal, Kobbie Mainoo wa Manchester United na Destiny Udogie.

Kocha Mikel Arteta wa Arsenal, Unai Emery wa Aston Villa, Pep Guardiola wa Manchester City, Andoni Iraola wa Bournemouth na Jurgen Klopp wa Liverpool watapigania tuzo ya Meneja Bora wa Msimu.