Real Madrid na Dortmund kumenyana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Juni 1

Real wamewahi kushinda Ligi ya Mabingwa mara 14 huku Dortmund wakiwa wamewahi kushinda mara moja pekee.

Muhtasari

•Real Madrid ilipiga Bayern Munich ya Ujerumani na kufuzu kwa fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza mnamo Juni 1,

•Real Madrid na Borrusia Dortmund sasa zitakutana kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza mnamo Juni 1.

Image: TWITTER// CHAMPIONS LEAGUE

Timu ambazo zitamenyana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa 2023/24 sasa zimeamuliwa..

Jumatano usiku, miamba ya soka ya Uhispania Real Madrid ilipiga Bayern Munich ya Ujerumani na kufuzu kwa fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza mnamo Juni 1, 2024.

Sasa wanaungana na Borrusia Dortmund waliofuzu kwa fainali siku ya Jumanne usiku baada ya kuwashinda wababe wa soka wa Ufaransa Paris Saint Germain (PSG).

Borrusia Dortmund ilipiga PSG nyumbani na ugenini na kupata nafasi ya kufuzu kwa fainali. Katika kila mechi, walifunga bao moja huku mpinzani wao akishindwa kufunga bao lolote. Mshambulizi Niclas Fullkrug alifunga bao la ushindi katika mchuano wa kwanza nyumbani huku beki Mats Hummels akifunga bao la ushindi katika mechi ya mkondo wa pili iliyochezwa nchini Ufaransa siku ya Jumanne usiku.

Kwa upande mwingine, Real Madrid na Bayern Munich zilitoka sare ya 2-2 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa nchini Ujerumani wiki iliyopita huku miamba hao wa Uhispania wakishinda 2-1 katika mechi ya mkondo wa pili iliyochezwa Santiago Bernabeu Jumatano usiku.

Mshambulizi Joselu aliifungia Real Madrid mabao yote mawili katika kipindi cha pili baada ya beki Alphonso Davies kufungia wapinzani wao kutoka Ujerumani bao la kwanza katika kipindi cha kwanza.

Real Madrid na Borrusia Dortmund sasa zitakutana kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza mnamo Juni 1 wakati mshindi wa kombe la mwaka huu atakapojulikana.

Miamba hao wa Uhispania wamewahi kushinda Ligi ya Mabingwa mara kumi na nne huku Borrusia Dortmund wakiwa wamewahi kushinda kombe hilo mara moja pekee.