'Ndovu' acheza ngoma nyumbani kwa adui mkubwa huku akiwapa presha Man City

Wanabunduki walikuwa wameshinda ugani Old Trafford mara moja tu kwenye ligi ya tangu 2006.

Muhtasari

•Arsenal iliwashinda Man United na kupata pointi tatu muhimu siku ya Jumapili jioni huku Ligi Kuu ya Uingereza ikikaribia kumalizika.

•Msimu wa EPL 2023/24 utakamilika Jumapili, Mei 19 wakati mshindi wa kombe hilo atakapojulikana.

 

Image: TWITTER// ARSENAL

Wanabunduki waliwashinda wapinzani wao wa muda mrefu Manchester United na kupata pointi tatu muhimu siku ya Jumapili jioni huku Ligi Kuu ya Uingereza ikikaribia kumalizika.

Ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Arsenal katika uwanja wa Old Trafford ndani ya takriban miaka minne.

Klabu hiyo yenye maskani yake London ilikuwa imeshinda ugani Old Trafford mara moja tu kwenye ligi ya tangu 2006, na hiyo ilikuwa mnamo Novemba 2020 kwenye uwanja usio na mashabiki wakati wa msimu wa 2020-21 ulioathiriwa na janga la Covid-19.

Mshambulizi wa Ubelgiji Leandro Trossard alifunga bao la pekee katika mechi hiyo ya kusisimua na kuwapa vijana wa Mikel Arteta ushindi muhimu wa 0-1. Alifunga bao hilo kupita kipa Andre Onana katika dakika ya 21 akimalizia pasi maridadi ya kiungo Kai Havertz.

Ushindi wa Jumapili jioni uliwarudisha wanabunduki kileleni mwa jedwali huku wakisubiri kuona jinsi washindani wao wakuu wa msimu huu, Manchester City wanavyocheza katika mechi zao mbili zilizosalia.

Arsenal sasa ina pointi 86 kati ya michuano 37 waliyocheza, huku vijana wa Pep Guardiola wakiwa na pointi 85 katika mechi 36, walizocheza hadi sasa. Iwapo timu zote mbili zitashinda mechi zao zilizosalia, Arsenal kwa bahati mbaya italazimika kushika nafasi ya pili kwa mara ya pili mfululizo.

Msimu wa EPL 2023/24 utakamilika Jumapili, Mei 19 wakati mshindi wa kombe hilo atakapojulikana.

Man City bado wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya Tottenham ambao utachezwa Jumanne, Mei 14 kabla ya kukutana na West Ham nyumbani Mei 19.

Kwa upande mwingine, wanabunduki watamenyana na Everton kwa mechi yao ya mwisho Mei 19.

Je, nani ataenda nyumbani na kombe la EPL 2023/24?