Utata huku aliyekuwa mchezaji wa Barcelona akidaiwa kumtuma kakake pacha kumchezea

Edelino alidaiwa kuingia uwanjani akijifanya pacha wake siku ya Jumapili iliyopita.

Muhtasari

•Edgar alishutumiwa kwa kumtuma pacha wake Edelino Le kuichezea klabu ya Dinamo Bucharest, badala ya kwenda huko mwenyewe.

•Klabu imesema alisainiwa kupitia wakala mashuhuri wa michezo wa Uropa na kwamba uwazi na uhalali ulitawala katika mchakato wote.

Mchezaji Edgar Le
Image: HISANI

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Barcelona amejikuta katika hali ya kutatanisha ambapo anakabiliwa na tuhuma za ulaghai.

Edgar Le ambaye aliichezea timu ya akiba ya Barcelona takriban muongo mmoja uliopita alishutumiwa hivi majuzi kwa kumtuma pacha wake Edelino Le kuichezea klabu ya Dinamo Bucharest, badala ya kwenda huko mwenyewe.

Tetesi zilianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii baada ya mwandishi wa habari wa Romania Emmanuel Rosu kuripoti kwamba duru za ndani za klabu hiyo zinaamini kwamba alimtuma pacha wake Edelino kucheza badala yake.

Taarifa hizo zilidai kuwa Edelino aliingia uwanjani akijifanya pacha wake siku ya Jumapili iliyopita katika mechi kati ya Dinamo Bucharest na FC UTA Arad, inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Romania.

Dinamo Bucharest hata hivyo mnamo Jumatatu ilikanusha madai hayo na kueleza kuwa habari hizo ni za uongo. Klabu hiyo pia ilitangaza hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari hizo.

"Ni habari za uwongo, ni kashfa na mbaya dhidi ya klabu," timu hiyo ilisema katika taarifa yake kujibu uvumi huo ulioanza kwenye mitandao ya kijamii kwamba.

Klabu hiyo ilikanusha taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba Edelino, na si Edgar, alijiunga na klabu hiyo Februari mwaka jana kutoka Feyenoord ya Uturuki.

Ilibainisha kwamba Edgar Ie alisainiwa kupitia wakala mashuhuri wa michezo wa Uropa na kwamba uwazi na uhalali ulitawala katika mchakato wote.

Akiwa ameanzia kucheza Barcelona, ​​Edgar Ie pia amechezea vilabu vya Villarreal, Lille, Nantes, Trabzonspor na Feyenoord.

Le ni mchezaji wa kimataifa wa Guinea-Bissau, na tangu acheze kwa mara ya kwanza chini ya Luis Enrique akiwa na Barcelona amepitia timu za Villarreal, Lille, Feyenoord, Nantes, Trabzonspor na kisha Basaksehir kabla ya kusajiliwa Dinamo msimu huu wa joto.

Wakati Edgar ametumia muda mwingi wa maisha yake kuzunguka ligi kuu za Uropa, Edelino kwa upande wake alisaini Resende ya Ureno baada ya kuacha akademi ya Sporting CP. Timu yake ya mwisho kujulikana ilikuwa Tluchowia Tluchow nchini Poland.